SMZ yaipongeza WB kudhamini miradi

NA MWINYIMVUA NZUKWI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali, ameipongeza Benki ya Dunia (WB) kwa misaada na mikopo inayoipatia Zanzibar kwani imechangia kuimarisha ustawi na maendeleo ya jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo kanda ya Afrika, Dk. Taufila Nyamadzabo, ofisini kwake Vuga, alieleza kuwa miradi mbali mbali iliyoidhinishwa na benki hiyo hivi karibuni itachochea kasi ya maendeleo ya Zanzibar na watu wake.

Alieleza kwamba ili kufikia malengo iliyojiwekea, Zanzibar inapaswa kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na washirika wa maendeleo jambo ambalo alimuahidi mkurugenzi huyo kulisimamia kikamilifu.

“Miradi iliyoidhinishwa na Benki ya Dunia ina sura mbili, yaani msaada na mikopo nafuu, hivyo ili tufanikiwe lazima tuwe na usimamizi bora ili tija ipatikane,” alieleza Jamal.

Akiitaja miradi iliyoidhinishwa na WB ambayo ilikuwa ni sehemu ya mazungumzo yao kuwa ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya umeme (ZESTA) wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 142.

“Mradi huu unakwenda kuongeza upatikanaji wa umeme hasa katika maeneo ya kusini na kaskazini ya kisiwa cha unguja kwani vituo vya umeme mkubwa vitajengwa na kuondoa changamoto ya umeme mdogo katika maeneo hayo,” alieleza Jamal.

Alifafanua kwamba mradi huo unahusisha ujenzi wa mfumo wa usafirishaji wa umeme kwa kujenga njia ya umeme wa KV 132 na kuongeza uwezo wa usambazaji wa huduma hiyo.

Aliutaja mradi mwengine ni wa uimarishaji wa mji wa Zanzibar unaotambuliwa kama BIG Z uliotengewa Dola 150 ambao utahusika na ujenzi wa barabara, uwekaji wa mifumo ya maji taka, kuweka taa za barabarani, kupendezesha mji na kumalizia kazi zilizobakia kwenye mradi wa huduma za jamii (ZUSP).

Aidha Jamal alieleza kuwa katika mazungumzo hayo waliwasilisha maombi kwa mkurugenzi huyo kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya watendaji kutoka Zanzibar katika ofisi za benki hiyo na mashirika mengine ya kimataifa ili kuwajengea uwezo lakini pia kuhaulisha uzoefu wao wanaporudi kufanya kazi nchini.

Akizungumza katika mkutano huo uliowajumuisha katibu mkuu wa wizara ya fedha Zanzibar Dk. Juma Malik Akil na naibu katibu mkuu wizara ya fedha na mipango ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Amina Khamis Shaaban, Dk. Nyamadzabo, alisema benki ya dunia imeridhishwa na utekelezaji wa miradi wanayoifadhili.

Alieleza kuwa kwa kipindi kirefu fedha zinazotolewa na WB kwa miradi mbali mbali ya kijamii, zimekuwa zikitumika vyema na kuleta tija kwa wananchi jambo lililopelekea Tanzania kuidhinishiwa fedha za mikopo na misaada.

“Hivi karibuni tumeidhinisha fedha kwa ajili ya mkopo na msaada kwa ajili ya Tanzania kwenye miradi ambayo itachochea kasi ya maendeleo ya nchi na watu wake, hili ni jambo jema na mara zote Tanzania imekuwa ikibuni miradi yenye tija,” alisema Dk. Nyamadzabo.

Mkurugenzi huyo, alimpongeza waziri jamal kwa kuwasilisha vyema bajeti ya serikali ambayo alisema imeakisi mahitaji ya jamii na maendeleo ya nchi kuelekea na kueleza kuwa benki hiyo itaendelea kufadhili miradi iliyoombwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango