Tuwafunzwe watoto wetu kuyapenda, kuyatunza mazingira - DC Msaraka
NA SALUM VUAI
MKUU
wa Wilaya ya Mjini, Rashid Simai Msaraka, jana alizindua wiki ya maadhimisho ya
siku ya mazingira duniani, huku akiihimiza jamii kuwajengea watoto mapenzi na
muamko wa kupanda na kutunza miti.
Maadhimisho
ya siku hiyo yanayofikia kilele chake tarehe 5 Juni, yanafanyika kwa harakati
mbalimbali zinazohusisha uhifadhi wa mazingira ya nchi kavu na baharini.
Katika
uzinduzi huo uliofanyika kwenye bustani ya Botanic iliyopo Migombani Wilaya ya
Mjini, Msaraka aliongoza wananchi mbalimbali na wadau wa mazingira, katika
shughuli ya kupanda miti kwa lengo la kulistawisha eneo hilo.
Akizungumza
na wananchi wakiwemo wanafunzi wa skuli ya msingi Migombani, Mkuu huyo wa
Wilaya alisema ni muhimu wazazi na walezi kuwarithisha watoto utamaduni wa
kuyapenda mazingira kwa kujumuika nao katika upandaji miti mbalimbali ikiwemo
ya matunda na kivuli.
Alisema
miti ni rasilimali inayopaswa kuendelezwa kutokana na faida zake kwa jamii
ambazo zinabaki kuwanufaisha watu na viumbe vyengine hata pale wanapoipanda na
kuistawisha wanapokuwa wametangulia mbele ya haki.
Alisema
kupanda miti na kuhifadhi mazingira ni sehemu ya ibada ambayo mtu akifanya
anapata fungu kwa Mwenyezi Mungu, akitoa mfano wa kiongozi wa Waislamu Mtume
Muhammad (S.A.W) ambaye wakati kukiwa na vita aliwasisitiza wafuasi wake
wasikate miti ovyo au kuharibu mimea.
Alifahamisha
kuwa, jamii inapowekeza kwa kuwarithisha watoto mambo yenye manufaa, ni
kutafuta rehema za Muumba kwani hata miti iliyopo sasa imepandwa na watu wa
kale ambao wameshafariki, lakini wanaofaidi ni kizazi cha sasa na wao wanapata
thawabu.
Aliwapongeza
vijana wa Shehia ya Migombani kwa hatua ya kujikusanya na kuunda jumuiya yenye
lengo la kulibadilisha eneo la bustani ya Botanic, kutoka lilivyokuwa makao na
maficho ya wahalifu na watumiaji dawa za kulevya, na kuligeuza kuwa eneo la
kiuchumi na kupumzikia.
Comments
Post a Comment