Wananchi Kaskazini Unguja wapongeza GNU

NA KHAMISUU ABDALLAH

WANANCHI wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wamepongeza hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kutekeleza katiba na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) iliyoimarisha umoja wa Wazanzibari.

Wananchi hao walitoa pongezi hizo katika mkutano ulioandaliwa na Rais Mwinyi kwa ajili ya kuwashukuru kwa kumchagua kwa asilimia 100 ya kura katika uchaguzi uliofanyika 2020 katika ukumbi wa Ofisi ya chama hicho Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda.

Walisema katika miaka ya nyuma hasa mkoa huo uliweka matabaka baina ya vyama na vyama mtu na mtu jambo ambalo lilikuwa halileti taswira njema hasa kwa dini ya kislaamu.

Aidha walisema kitendo alichokifanya Rais kimeonesha imani kubwa kwa wananchi wa Zanzibar katika kuona wanakuwa wamoja kwani hakuna jambo jema kama kuwaunganisha watu waliogombana.

“Watu wa Kaskazini tunakupongeza kwa dhati kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwani hivi sasa sote ni wamoja,” walisema.

Maryam Ali kutoka kijiji cha Bumbwini Makoba alisema siasa za nyuma zilikuwa na mfarakano mkubwa baina ya mtu na mtu kutokana na siasa kuwa za chuki na ubaguzi.

Alisema siasa za zamani watu walikuwa hawazikani, hawatembeleani, hawauziani bidhaa na hata watu kuchagua misikiti mambo ambayo hivi sasa yote yameondoka.

Aidha alisema jambo alilofanya rais kuunda serikali hiyo ni la kupongezwa kwani ameweza kuwaunganisha wazanzibari kuwa wamoja.

Naye Ali Khamis alisema siasa za zamani wazanzibari walikuwa sio wamoja hali ambayo ilikuwa ikiwawia vigumu hasa wanaCCM katika Mkoa wa Kaskazini.

Alisema watu wa Mkoa huo wana imani sana na yeye katika kuyatekeleza yale yote ambayo waliyoyapanga katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.

Hivyo, waliahidi kumuunga mkono katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo sambamba na kusimamia suala la amani na utulivu wa nchi yao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema alipoingia madarakani aliamua kufanya utaratibu wa kuondoa ugomvi, mifarakano, fujo ndani ya nchi na kuwaunganisha wazanzibari kuwa wamoja kama wananchi wa Zanzibar na kuwa na amani kwa maslahi ya maendeleo ya nchi yao na vizazi vya sasa na baadae.

Aisema nchi haiwezi kupata maendeleo bila ya kuwa na amani hivyo aliamua kutengeneza serikali ya umoja wa kitaifa kwa kufuata matakwa ya kikatiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Aidha alisema katika kuunda serikali hiyo hawakuzozana bali walijadili na kuona jambo hilo lina kheri kwa watu wote na vyama vyote kwa kukutana na kuungana ili kupata amani na kuijenga nchi yao.

Dk. Mwinyi alisema wananchi wanakumbuka ilivyokuwa nchi yao kwani watu walikuwa hawazikani, misikiti wanachagua, watu wanaachwa kwa kupewa talaka watu katika kipindi cha uchaguzi lakini mambo hayo sasa hakuna na wananchi wako kwenye amani na kilichobaki ni kuleta maendeleo ya watu.

Hata hivyo, Rais Mwinyi, aliwapongeza wananchi wa Mkoa huo kuweka historia ya ushindi kwa chama chao kuanzia nafasi ya Wawakilishi, Udiwani, Ubunge na Urais.

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango