Watakiwa kuzingatia viwango kwenye kazi za ubunifu, utamaduni

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, amesema serikali kupitia wizara yake inaunga mkono ushiriki wa mashindano yaliyoanzishwa na taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) kwani yataiwezesha Zanzibar kuwa kwenye ramani ya ulimwengu wa viwango.

Alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la insha inayohusu mchango wa Viwango, Sanaa, Utamaduni na Urithi Jamii katika kukuza uchumi bunifu barani Afrika iliyoandaliwa na shirika la viwango Afrika (ARSO), hafla iliyofanyika katika jengo la ZURA, Maisara Zanzibar.

Alisema inaposhiriki katika mashindano na shughuli za mashirika ya kimataifa na kikanda, kwa asilimia kubwa inaweza kufanya vizuri na kuaminiwa hivyo ni imani yake kwamba ZBS itaendelea kuwa wadau wakubwa wa shirikisho hilo la Afrika.

Akizungumzia maudhui ya mada ya mashindano hayo, Shaaban alisema, sanaa na ubunifu vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar hivyo aliwataka wanafunzi wasiishie kuandika insha pekee badala yake kusomea mambo ya viwango pindi watakapomaliza masomo kusaidia maendeleo ya nchi yao.

Hata hivyo, Waziri Omar, alibainisha kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya ubunifu na viwango katika mambo mbali mbali ikiwemo kupunguza gharama hasa katika mambo ya ujenzi.

Shaaban pia aliishauri ZBS kutoa elimu juu ya uhusiano baina ya ubunifu na viwango ili kuwawezesha watu kujua mambo muhimu katika mambo hayo ikiwemo wabunifu wa majengo, watu wa sanaa, mapishi na watu wengine katika jambo hilo.

Aliwahakikishia wanafunzi kuwa insha walizoziandika zitachukua nafasi ya kwanza barani Afrika na kuipa heshima nchi yao.

Katika hatua nyengine aliwapongeza walimu wa wanafunzi hao katika kuwasimamia na kuona wanafanya kazi nzuri ambayo imewawezesha kupata ushindi.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Rahima Ali Bakar, alisema mashindano hayo ni moja ya hatua ya kuelekea kilele cha shindano la insha na kusherehekea siku ya viwango Afrika na kuwapongeza wanafunzi na walimu kwa kushiriki shindano hilo na kupata washindi wengi zaidi.

Alisema mashindano hayo waliyoanza mwaka 2019 ambapo wanafunzi 16 walishiriki, mwaka 2020 washiriki walikuwa 18 na kwa mwaka huu washiriki walikuwa 33 idadi ambayo imekuwa ikiongezeka kila mwaka.

Aidha alisema katika mashindano ya jumuiya ya ARSO ya mwaka uliopita, Zanzibar ilipata mshindi wa saba hivyo aliwataka wanafunzi kushajihika na kutovunjika moyo katika kushiriki mashindano hayo.

Mkurugenzi huyo aliahidi yale yote yaliyoelekezwa na wizara katika jambo hilo watayachukua na kuyafanyia kazi ili kuweza kushiriki katika mashindano hayo barani Afrika.

Mkuu wa Mashirikiano na Uhariri wa Viwango wa ZBS, Kidawa Hassan, akiwasilisha mada kuhusu mchango wa viwango kwa sanaa, utamaduni na urithi, alisema viwango vina mchango mkubwa katika kitangaza bidhaa na nyenzo bora kwa wabunifu kuweza kupata soko nje ya nchi kupitia bidhaa zao wanazozizalisha.

Wanafunzi walioshiriki katika mashindano hayo waliahidi kuhakikisha wanajitoa katika kuandika insha mbalimbali na kuwashajihisha wanafunzi wenzao katika kushiriki mashindano mbalimbali nchini.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango