Wizara ya habari kuwaendeleza watendaji wake
- Yapongeza utendaji wa vyombo vya habari
WIZARA ya Habari, Vijana,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, imeeleza kuwa mwaka wa fedha 2021/2022, itaimarisha
mazingira ya utendaji kazi kwa wafanyakazi wake ikiwemo utoaji wa vitendea kazi
na stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
wizara hiyo, Tabia Maulid Mwita (pichani), wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato
na matumizi katika Baraza la Wawakilishi Chukwani, Juni 2, 2021.
Alisema mpango huo utaenda
sambamba na kuwaendeleza wafanyakazi hao kwa kuwapatia mafunzo ili kutekeleza
majukumu yao ya kila siku kwa lengo la kuongeza ufanisi na bidii ya kazi.
Aidha alisema wizara katika mwaka
huo pia imejipangia maeneo muhimu ya utekelezaji, ikiwemo kuimarisha
miundombinu ya habari kwa ajili ya uzalishaji wa vipindi, ununuzi wa maudhui,
ufatiliaji wa habari, ununuz wa mitambo ya uchapaji.
Waziri Tabia alieleza kuwa kipaumbele
chengine ilichojiwekea ni kuimarisha huduma za maendeleo ya vijana kwa
kuanzisha mfuko wa mikopo kwa vijana na kuanzisha vituo vya vijana.
“Wizara pia imejipanga kuimarisha
huduma za utamaduni kwa kujenga chuo cha utamaduni na kuanda mpango wa kuendeleza
lugha ya Kiswahli na kufuatilia fursa ziliopo za mahitaji ya Kiswahili ndani na
nje ya nchi,” aliongeza Tabia.
Tabia alieleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuongeza ajira na kukuza,
kuhifadhi na kuendeleza utamaduni, sambamba na ubunifu kwa jamii ya Zanzibar ili
haki na maslahi ya wasanii na wabunifu zipatikane.
Sambamba na hiyo alisema
wataimarisha miundmbinu ya michezo pamoja na kuviwezesha vyama vya michezo
kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sera, sheria ya baraza na mashirikisho ya
kimataifa, kikanda na kitaifa na kuzisaidia timu za taifa na za watu wenye
ulemavu.
Kuhusu programu ndogo ya
usimamizi wa vyombo vya habari, utangazaji na uchapaji alisema wizara imetenga
jumla ya shilingi 11,047,960,000 kwa lengo la kutoa matokeo ya muda mrefu na
kuleta usimamizi bora wa vyombo vya habari na upatikanaji wa habari zenye
maadili.
Aidha alisema wizara yake
imepanga kuwajengea uwezo wafanyakazi wa mashirika na kampuni yaliyomo ndani ya
wizara hiyo ili kuendana na kasi ya teknolojia inayokuwa kwa haraka duniani na
kuleta ufanisi katika kazi zao.
Mbali na hayo alieleza pia wizara
pia imepanga kuweka mazingira bora ya kazi kwa kuwapatia vifaa vya kisasa na
vinavyokwenda na wakati.
Akiwasiliasha maoni ya kamati ya
Ustawi wa Jamii kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka
2021/2022, Mjumbe wa kamati hiyo Zawadi Amour Nassor, alisema kamati inaishauri
wizara kukiimarisha kitengo cha masoko cha shirika la Magazeti ya Serikali
Zanzibar.
Alisema hatua hiyo itapelekea magazeti
ya shirika hilo yaweze kuwafikia wananchi kwa haraka na kusomwa na watu wengi
Zanzibar na Tanzania bara kwa ujumla.
Aidha alisema kamati imebaini
usambazaji na utoaji wa gazeti la Zanzibar leo hauridhishi kutokana na
kukosekana kwa masoko ya uhakika ndani ya Tanzania hali inayosababisha shirika
kuzalisha magazeti lakini mengi yanabakia ofisini kwa kukosa soko.
Hata hivyo kamati iliiomba serikali
ya awamu ya nane kuzitaka taasisi zote zinazodaiwa na Wakala wa Uchapaji (ZAGPA)
kulipa madeni hayo haraka kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara kwani kufanya
hivyo kutasaidia wakala kuondokana na ukakasi wa matumizi.
Katika mwaka wa fedha 2021/2022
wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 70,893,081,000 ambapo kati
ya hizo shilingi 14,424,100,000 ni kwa matumizi ya kawaida na shilingi
56,468,981,000 kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Comments
Post a Comment