Majaliwa aipongeza NMB kutekeleza mpango wa Ushirika Afya 

NA MWANDISHI WETU, TABORA

WAKULIMA nchini wametakiwa kutumia mpango wa Ushirika Afya ili kujihakikishia usalama wa afya zao wakati wa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, alipokuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Ushirika na kuitaja hatua hiyo kuwa ni mafanikio makubwa katika vita dhidi ya umaskini na maradhi.

Alisema makubaliano yaliyofikiwa kati ya benki hiyo na vyama hivyo vya ushirika, yanathibitisha kuanza rasmi kutolewa kwa huduma baada ya wanachama wake kukabidhiwa kadi za NHIF kwenye kilele Jumamosi iliyopita.

Aidha Waziri Mkuu alizishukuru taasisi za fedha kwa mchango inaoutoa kuviimarisha vyama vya ushirika na kuvifanya kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa.

Katika hafla hiyo, Majaliwa alikabidhi kwa wakulima wa tumbaku Kulwa Mfaume, Saleh Mpemba na Athanas Semeduke kadi za NHIF zilizofadhiliwa na NMB ikiwa ni miongoni mwa kadi 102 za kwanza zilizotolewa na benki hiyo na kuifanya kuwa ya kwanza kufanya hivyo.

Aidha, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema benki hiyo ina mpango wa kuongeza kiasi cha pesa kwa ajili ya mikopo ya wakulima ya bima ya afya.

Aliongeza kuwa NMB wakiwa wadau wakubwa wa serikali na benki inayohudumia zaidi ya Watanzania milioni nne nchi nzima, itaendeleza mpango huo ili kuhakikisha urahisi wa kupatikana kwa bima ya afya kwa wakulima wote wa tumbaku na mazao mengine nchi nzima.

Kwa mujibu wa Mponzi, pamoja na kuchochea kilimo chenye tija, sababu ya NMB kuwekeza katika mpango wa Ushirika Afya ni kuunga mkono juhudi za serikali katika jitihada zake za kufikia malengo ya Afya kwa Wote kupitia bima ya afya iliyoimarishwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, alisema kuwa mpango huo ulianzishwa mwaka 2018 lakini utekelezaji wake ulidorora kutokana na changamoto ya vipato vya wakulima ambayo sasa imetatuliwa na ufadhili wa NMB.

“Tunashukuru mpango huu sasa umepata mdau wa kuusukuma ili kufikia lengo la kutomuacha nyuma mtu yeyote kama yalivyo malengo ya kitaifa na kimataifa kwenye maswala ya afya,” alieleza Konga.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Batilda Buriani, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Louis Bura, alisema bila ya baraka na udhamini wa TCDC zoezi hilo lisingefaulu kwa kiwango cha sasa hivi.

Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti na Usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dk. Benson Ndiege, alisema ufadhili wa aina hiyo unaviongezea vyama vya ushirika thamani na utasaidia kuwashawishi wakulima wengi kujiunga navyo.

Alieleza utiaji saini wa makubaliano hayo kati ya vyama vya wakulima wa zao la tumbaku, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na NMB ni alama muhimu katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika iliyoazimishwa kitaifa mkoani Tabora.

NMB imekuwa taasisi ya kwanza ya kifedha nchini kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wakulima baada ya kuingia makubaliano ya kutoa huduma hiyo na vyama vikuu viwili vya ushirika mkoani Tabora ambapo jumla ya shilingi bilioni 5 zimetengwa kwa ajili ya kuwakopesha wakulima 300,000 nchi nzima.

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango