Waandishi wahimizwa kuepusha migogoro
NA ASYA HASSAN
WAANDISHI wa habari wametakiwa
kujikita katika uandishi wa habari zenye mnasaba wa kuleta amani katika jamii
kwa lengo la kuepusha migogoro inayoweza kusababisha vuruga ndani ya jamii.
Hayo yalisemwa na Meneja Mkaazi wa shirika
la Search for Common Ground, Hussein Sengu, alipokwa katika mafunzo ya
usuluhishi na ujenzi wa amani yaliyowashirikisha waandishi wa habari kupitia
mradi wa dumisha amani unaosimamiwa na shirika hilo.
Aliseama waandishi wa habari ni
watu watakao weza kuifanya jamii kuwa na Amani ama kuisababisha kuingia
matatani hivyo ni vyema kuzitumia kalamu na midomo yao kwa uweledi na ufanisi
ili kuona Amani iliyopo inazidi kuimarika.
Meneja huyo alisema lengo la
mafunzo hayo nikuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya namna ya kuripoti
habari zenye mlengo wa kuleta amani katika jamii na sio kuongeza tofauti
ziliyopo ndani ya maeneo yao.
Sambamba na hayo alisema jamii
imekuwa ikikabiliwa na matatizo tofauti hivyo ni vyema waandishi kuandaa mazingira
mazuri yatakayosaidia kuleta busara kwa jamii kuweza kupambanua na kuchanua
njia sahihi ya kuzitua ili kuondosha tofauti zao.
“Jamii imekuwa ikikabiliwa na
migogoro kisiasa hususani kipindi cha uchaguzi, migogoro ya ardhi na hata
migogoro ya kijamii kama ya udhalilishaji wa kijinsia, hivyo vyombo vya habari
vina wajibu wa kuhakikisha vinaripoti habari zenye malengo ya kuleta amani
katika jamii,” alisema.
Hata hivyo alifahamisha kwamba
endapo masuala hayo yasiposhughulikiwa ipasavyo yanaweza kuvuruga mfumo mzima
wa amani iliyopo hapa nchini na kuleta athari kwao na taifa kwa ujumla.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Kelvin
Pesambili, alisema waandishi wa habari wanapaswa kushiriki kikamilifu katika
eneo hilo ili kuona jamii inafika wakati inakaa pamoja na kuacha tofauti zao.
Kwa upande wao, baadhi ya waandishi
walioshiriki mafunzo hayo waliahidi kuwa mstari wa mbele kusaidia wananchi
hususani pale kunapotokezea migogoro ili waishi kwa amani.
Mradi wa dumisha amani Zanzibar ni
mradi wa miaka miwili, ambao unaendeshwa na taasisi ya Search for Common Ground
kwa kushirikiana na The Foundation for Civil Society ya Tanzania, chini ya
ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
Comments
Post a Comment