Waandishi watakiwa kuwasilisha kazi zenye ubunifu EJAZ
NA KHAMISUU ABDALLAH
KAMATI inayosimamia tuzo za umahiri
wa uandishi wa habari Zanzibar imeeleza haja ya waandishi kuzingatia ubunifu na
weledi katika kazi wanazoziwashilisha katika mashindano.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu
Mwenyekiti wa kamati hiyo inayoundwa na taasisi za habari Zanzibar, wakati
wakitangaza msimu wa pili wa tuzo hizo kwa mwaka 2021/ 2022 kwa waandishi wa
Zanzibar katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa wa Wizara
ya Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni Zanzibar.
Alieleza kuwa ili kazi iweze
kushinda, kuna haja ya mwandishi kufanya kazi ya ziada na kwamba upo umuhimu wa
kuzingatia misingi ya taaluma na matokeo ya kazi ya mwandishi.
“Tunawashukuru wote walioshiriki na
walioshinda katika msimu mwa kwanza na tunapoelekea msimu wa pili ipo haja ya
kujiandaa na kujipanga kikamilifu ili kazi yako hata kama haikushinda basi iwe
na matokeo,” alisema Dk. Mzuri ambae pia ni mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar.
Akitangaza tuzo zitakazoshindaniwa
kwa msimu wa pili, Katibu wa kamati hiyo, Imane Osmond Duwe, alisema tuzo hizo
zitatolewa kama ni sehemu ya kuthamini kazi zinazofanywa na wandishi wa habari
nchini.
Alisema tuzo hizo ni mwendelezo wa
tuzo zilizotolewa Mei 30, mwaka huu ambapo katika msimu wa pili zimeongezeka na
kufikia 11 badala ya tano za awali.
Alizitaja tuzo hizo kuwa ni ya uandishi wa
habari za uchumi wa buluu (tuzo ya Dk. Huseein Ali Mwinyi), tuzo ya uandishi wa
habari za jinsia na udhalilishaji (tuzo ya Maryam Mwinyi) na tuzo ya uandishi
wa habari za Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inayobeba jina la tuzo ya
Maalim Seif Sharif Hamad.
Imane alizitaja tuzo nyengine kuwa
ni ya uandishi wa habari za rushwa na uhujumu wa uchumi (tuzo ya ZAECA), tuzo ya uandishi wa habari
za kodi kwa maendeleo ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), tuzo za uandishi wa
habari za michezo, uandishi wa habari za uwajibikaji, uandishi wa habari za
afya, uandishi wa habari za utalii, uandishi wa habari za mazingira na
uandisihi wa habari wa haki za watoto.
“kamati inapenda kuwatangazia sekta
za tuzo mwakani zimeongezeka kutoka tano hadi 11 ikiwa ni ongezeko la asilimia
100 la sekta za ushingani,” alieleza katibu huyo.
Aongeza kuwa habari zitakazowasilisha
ziwe za uchunguzi ambazo zitakwenda kwa mfumo wa makala au habari za kawaida
zilizoandikwa kwa upana ikiwa ni matokeo ya utafiti mpaka uliofanywa kuhusu
masuala mbalimbali ya kisekta.
Hata hivyo alisisitiza kuwa kazi
zitakazowasilishwa ziwe zimechapishwa katika magazeti au vipindi vilivyorushwa
kwenye redio, televisheni za kawaida au za mtandaoni.
Akizungumzia vigezo vya kuzingatiwa
wakati wa kuandaa au kuwasilisha kazi hizo, alisema ni pamoja na ubora wa kazi
i, umuhimu wa kuzingatia uwiano sawa na jinsia na vyanzo vingi vya habari.
Vigezo nyengine ni ubunifu na
upekee wa mada husika, matokeo baada ya kutoka habari au kipindi, uwasilishaji
wa mada husika kimpangilio, ufasaha na mtiririko wa lugha, kuzingatia maadili
ya uandishi weledi na matumizi ya takwimu.
Aliongeza kuwa kwa upande wa
kipindi cha redio na televisheni kisizidi dakika 30 na picha na sauti ziwe
katika ubora unaostahiki huku akitoa fursa kwa makala inayozungumzia sekta
zilizoainishwa na taarifa zinazohusu Zanzibar zitakazorushwa na vyombo vya
Tanzania bara.
Aliongeza kuwa kazi zitakazopokelewa
ni zitakazotoka kuanzia Julai 2021 hadi Febuari 2022 hivyo aliwataka kukusanya
kazi zao au kuandika katika maeneo hayo na kwamba zitaanza kupokewa kuanzia
Machi 1 hadi 30, 2022.
“Tutambue kuwa sisi waandishi wa
habari ni kiungo na muhimili muhimu katika kuhamasisha na kuleta maendeleo kwa
ujumla katika taifa letu,” alibainisha.
Tunzo ya umahiri na weledi za
uandishi wa habari Zanzibar kwa mwaka 2021/2022 ni miongoni mwa matukio muhimu yatakayoenda
sambamba na na maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani ambayo
huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Mei 3 kila mwaka.
Kama ilivyo kwa mwaka huu, msimu wa
pili wa tuzo hizo zinaandaliwa na taasisi mbali mbali ikiwemo Baraza la Habari
Tanzania Zanzibar (MCT), Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Zanzibar (TAMWA
– Zanzibar), Klabu ya Waandishi wa habari Zanzibar (ZPC), ITV Zanzibar na Idara
ya Mawasiliano na Taaluma za Habari Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) na jumuiya
ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA).
Comments
Post a Comment