Kunambi ashukuru mchango wa NMB kuimarisha huduma za jamii
NA SHADYA SAID, WMA
MKUU
wa wilaya ya Magharibi ‘A’, Suzan Peter Kunambi, ameshukuru mchango unaotolewa
na sekta binafsi katika maendeleo ya huduma za jamii wilayani humo katika
nyanja tofauti.
Alieleza hayo wakati akitoa
shukrani baada ya kupokea msaada wa mabati 200 na vitanda 30 kwa ajili ya skuli
na vituo vya afya wilayani humo kutoka kwa benki ya NMB, hafla iliyofanyika
katika skuli ya Msingi Mbuzini.
Alisema msaada wa mabati unakwenda kutatua changamoto ya uhaba wa
madarasa katika skuli ya Mbuzini na skuli ya Mtoni Kigomeni kwani baadhi ya
madarasa yamekuwa yakihitaji kuezekwa ili kukamilisha ujenzi wa madarasa
ulioanza mwaka 2017.
“Kuchelewa kukamilika kwa madarasa
haya kumesababisha wananfunzi kusoma nje ya madarasa na vitanda hivi vinakwenda
kuongeza maeneo ya kupumzikia na kujifungulia katika vituo vyetu vya afya jambo
ambalo ni la kushukuriwa sana,” alisema Kunambi.
Aidha aliziomba taasisi nyengine
kuiga mfano wa benki hiyo ambayo ilisema imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii
na makundi yenye uhitaji jambo linaloongeza kuaminika kwake katika jamii.
Akikabidhi msaada huo wenye thamani
ya zadi ya shilingi milioni 30, Meneja wa biashara wa benki ya NMB Zanzibar,
Abdalla Duchi, alisema benki hiyo imekuwa mdau mkubwa kwa serikali katika
kuunga mkono juhudi za maendeleo.
Alieleza kuwa misaada inayotolewa
na benki hiyo maeneo mbali mbali nchini ni sehemu ya mpango wa benki hiyo
kurudisha sehemu ya faida wanayoipata kwa jamii ili kuimarisha huduma na ustawi
wa jamii.
“Fedha zinazotumika kama msaada
katika shughuli za maendeleo kama haya, asilimia 100 zinatokana na faida ya
kibiashara lakini pia kuthibitisha ukaribu wetu kwa jamii hivyo kuna umuhimu wa
kujiunga nasi kwani faida inayopatikana inawarudia na kuwanufaisha wao
wenyewe,” alieleza Duchi.
Akitoa maneno ya shukrani kwa niaba
ya walimu na watoa huduma za afya wilayani humo, Daktari Dhamana wa kituoa cha
afya Bumbwisudi, Dk. Said Fadhil, alisema vifaa vililivyotolewa vitatumika kama
vilivyokusudiwa kupunguza changamoto ya uhaba wa vifaa unaowakabili kwa muda
mrefu sasa.
Alieleza kuwa kwa muda mrefu baadhi
ya vituo vya afya na hospitali za wilaya hiyo zimekuwa zikikabiliwa na
changamoto ya vifaa jambo linalozorotesha huduma na kupelekea wananchi kufuata
huduma maeneo ya mbali.
“Tumefarajika sana na msaada huu,
kwani sisi kwenye afya tumekuwa na mahitaji ya vitanda vya kujifungulia na
vifaa vyengine kwenye vituo vyetu hivyo msaada huu unakwenda kupunguza
changamoto hiyo,” alieleza Dk. Said.
Katika hafla ya makabidhiano hayo,
DC Kunambi aliambatana na viongozi mbali mbali wa wilaya, manispaa ya magharibi
‘A’ na kamati za skuli na afya, alikabidhiwa mabati 200 na vitanda 30 ikiwa ni
mwendelezo wa misaada ya benki hiyo kwa huduma za jamii ambapo wiki iliyopita NMB
ilikabidhi msaada wa shilingi milioni 25 kwa sekta za elimu na afya za mkoa wa
Kusini Unguja.
Comments
Post a Comment