Waandishi andikeni habari zinazoepusha madhara
NA MWAJUMA JUMA
WAANDISHI
wa habari nchini wametakiwa kuongeza umakini katika utekelezaji wa majukumu yao
ili kuepusha madhara kwa watu wengine.
Wito huo umetolewa
na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) Abdallah Abdulrahman
Mfaume, wakati akifungua mkutano wa kukusanya maoni ya kutengeneza kanuni za
maadili ya uandishi wa habari na maudhui ya mitandaoni, uliofanyika katika ukumbi
wa Dk. Ali Mohamed Shein, uliomo katika jengo la ZURA, Maisara Zanzibar.
Amesema katika uandishi
na utangazaji wa habari kupitia vyombo habari mbali mbali, kuna haja ya
kuzingatiwa kwa ustaarabu na utamaduni wa nchi badala ya kuiingiza usataarabu wa
mataifa mengine sambamba na kuzihakikisha habari zinazitolewa.
“Kila nchi ina sheria
na kanuni zinazosimamia maswala ya habari pamoja na yale masharti ya jumla ya
kitaaluma, hivyo si vyema vyombo vyetu vikatumia kanuni za nchi nyengine na
ndio maana taasisi zetu kama UTPC (Muungano wa Klabu za Habari Tanzania) zinaandaa
kanuni kwa kushirikisha wadau wenyewe,” ameeleza Mfaume.
Aidha amesisitiza
haja ya wanahabari hasa za mitandaoni kuepuka kutoa habari zinazowadhalilisha
watu badala yake kujitahidi kupunguza madhara dhidi yaoHivyo alisema lazima wawe
makini katika utoaji wa habari zao mbali mbali ili kuepusha udhalilishaji kwa
wengine.
Washiriki wa
mafunzo hayo walisema waandishi wa habari mwanapojiwekea miongozo na kuifuata
katika kazi inasaidia na kurahisisha kazi zao za kila siku tofauti na kuwa na
kutokuwa na muongozo kwa wote.
Mwandishi wa DW, Salma
Said amesema pamoja na kufuatwa kwa maadili na miongozo inayotumia nchini, ipo
haja ya kuzingatiwa kwa matamko na miongpozo ya kimataifa inayosimamia mwenendo
wa habari nchini.
“Tukijiwekea na
miongozo yetu inayosimamia maswala yetu, itaturahisishia zaidi katika kufanya
kazi zetu bila ya migogoro au madhara kwetu, jamii na mamlaka zinazohusika,” amesema
Salma.
Ameongeza kuwa katika
mkutano huo, wamepata fursa ya kutoa maoni juu ya miongozo ambayo wanataaluma
wenyewe wanataka yawemo kwenye kanuni ikiwemo kutoandika habari za kushitua
ambazo zinaleta athari kwa watu wengine.
“Kimsingi mafunzo
haya yalilenga kwa watu wa mitandao ya kijamii ambayo hutoa picha mbaya za
kutisha hivyo katika mafunzo haya tumetoa maoni namna gani ya kuchapisha picha
ambayo inatisha au haipaswi kutolewa na watu kuiona”, alisema.
Nae mwandishi, Haji
Nassor kutoka mtandao wa ‘Pemba Today’ amesisistiza zaidi kufuata miongozo yao
ambayo wamejiwekea na itawasaidia katika kazi zao bila ya kumuathiri mtu
yeyote.
Amesema kwamba
Zanzibar kumekuwa na tatizo la utoaji wa habari katika vyombo mbali mbali hasa
zile za udhalilishaji ambazo huficha jina la mtoto aliyebakwa lakini hutajwa majina
ya wazee wake au mahala anayoishi au kusoma.
“Kufanya hivyo
humtambulisha mtoto jambo ambalo linalowafanya watoto kupata athari za
kisaikolojia za muda mrefu, sambamba na kuwafanya wanyanyapaliwe na wenzao,”
ameongeza.
Mapema Muwezeshaji
katika mkutano huo kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambilike,
alisema katika maandalizi ya kanuni hizo, mkazo mkubwa umewekwa kwenye mitandao
ya kijamii kutokana na kuwepo kwa mwingiliano wa hali ya juu kati ya vyombo vya
kawaida na vya mitandaoni.
“Tulipitia kanuni
za maadili ya uandishi wa habari kwa vyombo vyote lakini tumejikita zaidi
katika habari za kimtandao kutokana na kuwepo kwa muingiliano wa hali ya juu
kati ya vyombo hivyo lakini hata vyombo vya kawaida vinajielekeza huko,”
alisema.
Alisema
wanatayarisha kanuni hizo ili kuhakikisha kwamba wanachama wao wanakuwa na
miongozo ya kuwaongoza waandishi wa habari, jinsi ya kuandika habari
zinazozingatia maadili na taaluma ya uandishi wa habari.
Akizungumzia
mkutano huo, Katibu Mkuu wa ZPC, Mwinyimvua Nzukwi, alieleza kuwa mkutano huo
ni sehemu ya utekelezaji wa mradi kukuza uhuru wa habari na upatikanaji wa
taarifa unaotekelezwa kwa pamoja na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari
Tanzania (UTPC) na Shirika la International Media Support la Denmark (IMS), kwa
ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
Alieleza kuwa pamoja
na shughuli nyengine za mradi huo, klabu za waandishi wa habari kwa
kushirikiana na wadau wengine wa habari, wametakiwa kuandaa kanuni ambazo
zitatumika kusimamia mwenendo wa upashanaji habari nchini.
Comments
Post a Comment