Balozi Hamza ahimiza ushirikiano sensa ya majaribio
NA MWANDISHI WETU
KAMISAA
wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Zanzibar, Balozi Mohammed Haji Hamza, amewataka
wananchi wa shehia ya Michungwani, wilaya ya Magharib ‘B’, kutoa ushirikiano kwa
makarani wa sensa na kutoa taarifa sahihi katika sensa ya majaribio
itakayofanyika baadae mwezi huu.
Akizungumza
katika mkutano na wananchi wa eneo la Misufini, katika shehia
hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kukutana na viongozi wa serikali, kijamii na wananchi kwa
lengo la kutoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya ushiriki wa zoezi hilo.
Alisema
sensa ya watu na makaazi ndio njia pekee ya kupata taarifa za msingi zikiwemo za
idadi ya watu na taarifa mbali mbali za upatikanaji wa huduma za jamii zitakazotumiwa
na serikali na watunga sera kupanga mipango ya maendeleo ya nchi.
“Kikawaida
sensa hufanyika kila baada ya miaka 10 lakini kabla ya kuingia kwenye zoezi
lenyewe hufanyika majaribio mwaka mmoja kabla ili kupima hatua mbali mbali za matayarisho ya sensa hiyo,” alieleza Balozi Hamza.
Nae
Sheha wa Shehia hiyo, Fauzia Omar Mahawi, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa shehia
yake, alisema watakuwa mstari wa mbele kuhamasishana wananchi wa eneo
lililoteuliwa kufanyika kwa sensa hiyo ili washiriki kuwawakilisha wananchi wa
vshehia nzima.
Alisema
ili kuona kila mtu kwenye shehia anahesabiwa kwa lengo la kufanikisha zoezi
hilo, kamati ya shehia imejipanga kutoa kila aina ya ushirikiano kwa makarani
walioteuliwa pindi watakapofika katika shehia hiyo.
Zoezi
la sensa ya watu na makazi ya majaribio linatarajiwa kufanyika usiku wa Septemba
10 kuamkia 11, mwaka huu, ambapo maeneo mbali mbali yametengwa kufanyika kwa
majaribio hayo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sensa itakayofanyika mwakani
ambayo ni ya sita kufanyika tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baadhi ya wananchi wa shehia ya Michungwani wakiwa kwenye mkutano wa uhamasishaji wa sensa ya majaribio itakayofanyika baadae mwezi huu.
Comments
Post a Comment