BASFU yafanya msako wanaokiuka sheria
NA MWANDISHI WETU
KATIKA kukabiliana na changamoto ya
ukiukwaji wa maadili na sheria inayohusiana na upigaji wa muziki, Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni (BASFU), limefanya ukaguzi wa kushitukiza na
kubaini uwepo wa kumbi za starehe na baa zinazopiga muziki bila kuwa na leseni ya kufanya
hivyo.
Ukaguzi huo uliofanyika usiku wa kuamkia Septemba 11, 2021 katika maeneo mbali mbali ya shehia za Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja,
ulibaini uwepo wa maeneo na waendesha shughuli za muziki wanaofanya shughuli
hiyo kinyume na sheria.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo,
mrajisi wabaraza hilo, Juma Chum Juma, alieleza kuwa kufanya hivyo ni kinyume
na sheria namba 7 ya mwaka 2013 inayotoa maelekezo namna ya kuendesha shughuli
hizo.
“Kwa mujibu wa sheria ya baraza,
sehemu zote za burudani, biashara na maeneo ya umma yanakazwa kupiga muziki na
shughuli nyengine za burudani bila ya kuwa na leseni,” alieleza Juma.
Aliongeza kuwa hatua hiyo imelenga
kuimarisha ustawi wa jamii lakini pia kutoa utulivu kwa wakaazi wa maeneo ya
biashara jambo ambalo limekiukwa na wafanyabiashara hao.
Alifafanua kuwa katika maeneo 20
waliyoyakagua usiku huo, maeneo saba pekee ndiyo yaliyokuwa na leseni zilizo
hai na maeneo 13 leseni zao zilikuwa zimepitwa na muda.
“… hata hawa ambao leseni zao
zilikuwa ndani ya muda, bado tumewakuta na makosa ya kukiuka masharti ya leseni
yakiwemo ya kupitisha muda uliowekwa lakini pia kupiga muziki kwa sauti ya juu
na kuwa kero kwa wananchi,” alisema Juma.
Akizungumzia zoezi hilo, Katibu wa
sheha wa shehia ya Nungwi Banda kuu, Khamis Kibata Mussa, alieleza kuwa
kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili katika maeneo hayo kunakosababisjhwa na
upigaji wa muziki bila kufuata taratibu zilizowekwa.
“Baa nyingi hapa zinapiga muziki
kwa sauti ya juu lakini wakati mwengine hadi alfajiri badala ya saa sita usiku
jambo ambalo ni kero kwa wenyeji na wageni,” alieleza Kibata.
Nae meneja wa MT Inn Villa, Yussuf
Benela, ambae alikutwa akiwa hana leseni ya kuendeshea biashara ya muziki na
burudani, alieleza kuwa hakuwa na uelewa kama alitakiwa kuwa na leseni hiyo
mbali ya leseni ya biashara.
“Kwa kweli ndio mara ya kwanza
kusikia kama nilikuwa tunatakiwa kuwa na leseni ya kupiga mzii ingawa sisi hapa
huweka muziki kwa ajili ya wateja wetu,” alieleza Benela.
Nae meneja wa baa ya Cobra Chill,
Anna Marendu, alikiri kuendesha shughuli hizo na kuahidi kufuata maelekezo
aliyopatiwa.
“Hapa hatupigi muziki ila leo
kulikuwa na sherehe ya kuzaliwa ya mteja wetu lakini tuliikharisha, naomba
tupewe e;limu zaidi,” alieleza meneja huyo.
Katika operesheni hiyo iliyohusisha
wajumbe wa kamati ya ulinzi ya baadhi ya shehia za Nungwi, jeshi la polisi na
watendaji wa baraza hilo, Mrajis alliyafungia maeneo yote hayo pamoja na
kuwataka wamiliki wake kufika katika ofisi za baraza hilo kuanzia leo ili
kurekebisha kasoro zilizobainishwa.
Comments
Post a Comment