Majaliwa aridhishwa hatua ya ujenzi reli ya SGR

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa Majaliwa (pichani kushoto), amekagua mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar es Salaam hadi Kilosa, mkoani Morogoro na kueleza kuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana wakati akikagua maendeleo ya ujenzi ya mradi huo katika kituo cha Kwala kilichopo mkoani Pwani, ambacho kitatumika kama kituo kikuu cha kufanya matengenezo makubwa ya mabehewa na injini za treni.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukamilisha ujenzi wa miradi yote iliyoanzishwa, hivyo Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali yao, na tunawahakikishia mradi huu utakamilika kwa wakati,”alisema Majaliwa

Alieleza kuwa Maendeleo ya ujenzi huu yanatia matumaini na kazi inaendelea kwa ufanisi na eneo lililobaki la Pugu Dar es Salaam tunaamini litakamilika kwa wakati, nimeridhishwa na vituo vya abiria vilivyokamilika.

Aidha, Waziri Mkuu amewasihi wafanyakazi wa mradi huo kufanya kazi kwa ufanisi kwani lengo la Serikali ni kuufikisha mradi huo katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Katavi katika bandari ya Karema.

“Njia zote za reli tunataka ziwe za kisasa, hii pia itawezesha kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, nchi yetu ni ya kimkakati kwa sababu nchi zote za jirani zinategemea reli hii,” alieleza.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kupunguza muda wa safari, kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na mwanza.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Massanja Kadogosa, amesema hadi kufikia mwezi wa nane mwaka huu ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ulikuwa umefikia asilimia 93.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa ujenzi wa kipande cha pili cha Mradi huo kinachoanzia Morogoro hadi Makutopola (Singida) ulikuwa umefikia asilimia 70.11.

Alisema SGR ikikamilika itachochea mipango ya Serikali ya awamu ya sita katika kutekeleza sera ya viwanda na kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2025.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana