Sandra Nankomah, Lily Kadima kushiriki ‘Mashariki Music Festival’
NA
MWANDISHI WETU
WASANII
Sandra Nankomah na Lily Kadima kutoka Uganda wametajwa kuwa ni miongoni mwa
wasanii watakaoshiriki tamasha la muziki la ‘Mashariki Festival’,
linalotarajiwa kufanyika Zanzibar baadae mwezi ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Mratibu wa tamasha hilo, John Kagaruki,alieleza kuwa tamasha hilo linafanyika
kwa lengo la kupata fedha ziitakazosaidia maendeleo ya Chuo cha Muziki cha Nchi
za Majahazi (DCMA).
Kagaruki alieleza kuwa, pamoja na wasanii
hao, pia wasanii kutoka Kenya, Tanzania bara na Zanzibar wakiwemo wahitimu wa
chuo hicho watafanya maonesho ya muziki na kazi nyengine za sanaa.
Aliwataja wasanii na vikundi
vitakavyotumbuiza kuwa ni Fadhilee Itulya na Makadem kutoka Kenya, Msafiri Zawope
na Mopao Swahili Jazz kutoka Tanzania bara wakati Zanzibar ikiwakilishwa na
vikundi vya Siti and the band na Tara Jazz.
Alieleza kuwa mbali ya shughuli za
muziki na burudani, tamasha hilo pia litaenda sambamba na maonesho ya bidhaa za
kilimo zinazofanywa na wajasiriamali wa Zanzibar.
“Tamasha pia litahusisha soko la
bidhaa lijulikanalo kama ‘Kwetu Kwao’ ambalo kikawaida hufanyika kila Jumamosi ya
kwanza ya mwezi huko Nyamanzi katika eneo la ujenzi wa Fumba Town,” alieleza
mratbu huyo.
Aidha Kagaruki aliishukuru kampuni
ya CPS Ltd kwa kudhamini tamasha hilo na kuwaomba wadau wengine kufanya hivyo
ili kufanikisha tamasha.
“Kwa kiasi kikubwa CPS wamechangia
kuwepo kwa tamasha hili ambalo linaratibiwa na chuo lakini wasanii
watakaoshiriki walikubalii kuchangia ikiwa ni pampoja na kukubali malipo sawa,”
alieleza.
Akizungumzia sababu za kudhamini
tamasha hilo, Afisa Mtendaji wa kampuni ya CPS, Tobias Dietzold, alieleza kuwa
imetokana na azma ya kampuni hiyo kuendeleza utamaduni wa Zanzibar na watu
wake.
“Wakati wote kampuni yetu ipo
mstari wa mbele kusaidia watu kudumisha na kuendeleza utamaduni wao na ndio
maana hatukusita kutoa mchango wetu japo ni mdogo,” alieleza Tobias.
Tamasha hilo linalotarajiwa
kufanyia Oktoba 2 na 3, mwaka huu Ngome Kongwe, linakuwa tamasha la kwanza
kuandaliwa na DCMA kwa kushirikisha wasanii wa ndani na nje ya Zanzibar ikiwa
ni sehemu ya njia za kukusanya fedha za maendeleo ya chuo hicho kilichoanzishwa
mwaka 2020.
Comments
Post a Comment