Vyombo vya habari vyatakiwa kuzipa kipaumbele habari za viongozi wanawake

NA MWINYIMVUA NZUKWI

VYOMBO vya habari vimetakiwa kuongeza jitihada za kuwahamasisha wanawake kujiandaa kuwania nafasi za uongozi ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa na uwakilishi sawa baina ya wanawake na wanaume kwenye vyombo vya maamuzi.

Wito huo umetolewa na Mtafiti wa maswala ya habari na mawasiloiano, Dk. Aboubakar  Rajab (pichani), alipokuwa akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu habari zinazowahusu wanawake viongozi, katika ofisi za Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA – Zanzibar), Tunguu, wilaya ya Kati Unguja.

Alieleza kuwa katika kipindi cha mwezi novemba na disemba 2020, vyombo vya habari viliripoti kwa uchache habari za viongozi wanawake ikilinganishwa na viongozi wanaume jambo linanoibua hisia za upendeleo.

Alisema ili kurekebisha hali hiyo, vyombo vya habari vinapaswa kuwa na mikakati madhubuti ya kuwajengea uwezo wanawake kuwa viongozi kwa kueleza mafanikio na changamoto zinazowakabili.

Alieleza kuwa utafiti huo ulihusiasha magazeti ya Zanzibar leo, Mwananchi, televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC TV), Zanzibar cable (ZCTV) na mitandao ya kijamii ya pemba today na ktv, vyote viliripoti kwa chini ya asilimia 50 ya hyabari na vipindi vilivyohusisha wanawake ikilinganishwa na wanaume.

“Kwa mfano katika kipindi cha utafiti, tumegundua kuwa ni asilimia 14 pekee ya habari zilizochapishwa katika gazeti la Zanzibar leo zilizohusiusha viongozi wanawake wakati gazeti la mwanachi halikuwa na habari za wanasiasa wanawake wa Zanzibar,” alieleza Dk. Aboubakar.

Aliongeza kuwa hali kama hiyo imehitokeza katika vyombo vyengine huku habari kuhusu wanawake viongozi zikipewa uzito mdogo.

“Najua kuna mambo mengi yanayochangia hili lakini kama wataalamu tunapaswa kuchukua hatua na kuwashawishi wakuu wa vyombo vyetu kutoa uzito sawa kwa habari zinazowahusu wanawake na wanaume ili kuwa na uwiano unaolingana,” alisema.

Awali akifungua mkutano huo ulioshirikisha waandishi na wahariri wa habari, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dk. Mzuri Issa Ali, alieleza kuwa utafiti huo umelenga kuonesha namna vyombo vya habari vinavyomuangalia mwanamke.

Alisema matokeo ya utafiti huo yakitumia vizuri, yataimarisha utekelezaji wa kazi za vyombo hivyo lakini pia kutanua wigo wa utoaji na upatoikanaji wa habari zinazowahusu wanawake kupitia vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa utafiti huo ni utekelezaji wa mradi wa ushirikishaji wanawake katika uongozi ambao unalenga kuwashajihisha wanawake kusimama na kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao kupitia vyama vyao.

“Ili kuongeza idadi ya wanawake wanaokwenda kugombea nafasi katika majimbo na kushinda ni lazima kuwajengea uwezo hivi sasa lakini kupitia vyombo vya habari tunaweza kwenda mbali zaidi ya kwenye nafasi hizi za kisiasa,” alieleza Dk. Mzuri.

Nao baadhi ya washiriki wa mkutano huo, waliahidi kutumia matokeo ya utafiti huo kubadilisha mwenendo wa utoaji wa habari kwenye vyombo vyao ili kufanikisha malengo ya usawa wa kijinsia.

Walieleza kuwa pamoja na utayari wa vyombo hivyo bado kuna changamoto ya utayari wa baadhi ya viongozi wanawake kutumia vyombvo vya habari hasa redia na televisheni.

Walieleza kuwa hali hiyo inatokana na woga na kasumba inayoshinikizwa na uwepo wa mfumo dume uliotamalaki kwa muda mrefu katika jamii.

Mradi wa kuwajengea uwezo na ushawishi wanawake kuwania nafasi za uongozi unatekelezwa kwa pamoja kati ya TAMWA Zanzibar, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana