Tanzania inatambua kazi zinazofanywa na UN – Dk. Tax

NA SAIDA ISSA, DODOMA
JAMHURI  ya Muungano wa Tanzania imesema inatambua kazi kubwa inayofanywa na Umoja wa Mataifa (UN) ikiwemo ya kuimarisha umoja, mshikamano na ustawi wa jamii.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa jijini Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, alisema kuwa siku hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Alieleza kuwa maadhimisho hayo yanayofanyika kila mwaka yanalenga kutambua kazi zinazofanywa na umoja huo katika mataifa mbali mbali ulimwenguni ikiwemo Tanzania.

"Katika kipindi cha miaka 76 Umoja wa Mataifa umejitanabaisha kuwa ni taasisi muhimu kimataifa kutokana na mchango mkubwa katika masuala mabli mbali ya kimaendeleo, kijamii na amani ulimwenguni," alisema Waziri huyo.

Alieleza kuwa katika kipindi hiki dunia ikiwa inapambana na mlipuko wa UVIKO 19, ambao umesababisha changamoto nyingi na kuathiri dunia nzima katika sekta mbali mbali ikiwemo ya Afya ambayo mifumo yake bado haijitoshelezi.

"Janga hili limeendelea kutishia ustawi wa sekta za kijamii na uchumi kama vile usalama wa chakula,maji,lishe,biashara,utalii na sekta ya usafirishaji na hivyo kuathiri maendeleo ya uchumi kiujumla," alieleza.

Aidha alisema kuwa serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza Mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mapambano dhidi ya UVIKO 19 uliozinduliwa hivi karibuni ili kuikabiliana na makali ya ugonjwa huo.

Alieleza kuwa katika kukabiliana na UVIKO 19 Tanzania inaendelea kuchukua tahadhari mbali mbali kwa kudhibiti na kujikinga na ugonjwa huo kulingana na miongozo ya Shirika la afya Dunia ambapo umoja wa mataifa umekuwa mstari wa mbele kupambana na changamoto.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka alisema kuwa mkoa huu ulipokea chanjo 50,000 na wananchi wa mkoa wa Dodoma walichanja na chanjo ikaisha,pia wakaongezewa chanjo 1,500 kutoka mkoa wa Iringa ambazo zilimalizika na kuitishwa chanjo 1500 ambazo pia pia zilimalizika.

"Viongozi wa mkoa wa dodoma tumejitahidi kutoa elimu kwa kushirikiana na viongozi wa dini na viongozi wengine pamoja na makundi mbalimbali ikiwa ni kuendelea kuelimisha wananchi umuhimu wa chanjo," alisema Mtaka.

Aidha aliishukuru Serikali kwa namna ambavyo inaonesha jitihada kwa mapambano dhidi ya UVIKO 19 pamoja na mashirika mbali mbali ikiwemo Umoja wa Mataifa.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango