TASAF yaidhinishiwa 5.5b/- kukabili athari za UVIKO 19
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Ladislaus Mwamanga, amesema mfuko huo
umeidhinishiwa shilingi bilioni 5.5 kati ya fedha zilizotolewa mkopo wenye
masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Kimataifa (IMF).
Mwamanga
alieleza kuwa TASAF itazitumia fedha hizo kuondoa athari za kiuchumi
zilizochochewa na mripuko wa UVIKO 19 kwa kaya 40,740 za walengwa wa TASAF, wenye
uwezo wa kufanya kazi katika miradi ya jamii wanaoishi Mjini.
Alieleza
hayo jana katika ofisi za jijini hapa, wakati akizungumza na wandishi wa habari
katika ofisi za mfuko huo kuhusiana na Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa
Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19 kwa mpango wa kunusuru kaya za
walengwa wa TASAF.
Alisema
kupitia hizo kaya za walengwa wenye uwezo wa kufanya kazi wanaoishi katika
maeneo ya mjini, watafanya kazi katika miradi ya jamii na kulipwa ujira wa
wastani wa shilingi 135,000 kwa kila kaya ili kufufua au kuimarisha shughuli
zao za kukuza uchumi wa kaya zao zilizoathirika zaidi kutokana na UVIKO 19.
Aliongeza
kuwa, serikali imedhamiria kuwaondoa wananchi wake katika umaskini wa kipato
kwa kuwapatia ruzuku za kujikimu, ajira za muda, na kuwaongezea ujuzi, maarifa
na elimu ya ujasiriamali ili wakidhi mahitaji yao.
“Fedha
zilizotengwa kwa ajili ya TASAF ambayo ni shilingi 5.5 zitaelekezwa katika
utoaji wa ruzuku na utekelezaji wa miradi ya ajira za muda kwa kaya za walengwa
ili kupata kipato ambacho kitaziwezesha kaya hizo kujikwamua kiuchumi na
kupunguza athari za UVIKO - 19 na kuongeza rasilimali na miundombinu ambayo
itatumia na Jamii yote katika Mitaa na Shehia,” alisema.
Alisema
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuteleleza mipango na
mikakati mbali mbali katika kupunguza umasikini wa Watanzania na inafanya
jitihada za kupata fedha kutoka vyanzo vya ndani, mikopo na misaada kutoka kwa
wadau wa maendeleo ili kuhakikisha watu wanaondokana na umasikini.
“Utoaji
wa sehemu ya mkopo huo nafuu kwa ajili ya Mpango wa TASAF ni kielelezo tosha
kwamba serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu
Hassan, inawajali wananchi wake hasa wale wanaoishi katika mazingira duni,”
alisema Mwamanga.
Alisema
Walengwa hao watatekeleza miradi ya ajira ya muda itakayochangia kuongeza
upatikanaji wa chakula na kuboresha huduma katika sekta za afya, elimu, maji na
hifadi ya mazingira.
Mwamanga
alisema usimamizi utafanyika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango na
thamani ya fedha iliyotengwa, kwa ajili ya kusisimua uchumi wa kaya uliokuwa
umedorora kutokana na UVIKO – 19.
Comments
Post a Comment