UN kusaidia utatuzi changamoto mifumo ya afya

NA MWANDISHI WETU
UMOJA wa Mataifa (UN) Tanzania umeeleza kuridhishwa na ushirikiano uliopo baina ya serikali za Tanzania katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii.

Hayo yameelezwa na watendaji masjhirika ya umoja huo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Umoja wa Mataifa Kinazini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shughuli za maadhimisho ya miaka 76 toka kuasisiwa kwake.

Walieleza kuwa mashirika ya umoha huo, yanakusudia kushirikiana na serikali kuimarisha mifumo ya afya ili kuhamasisha jamii kuondokana na maradhi mbali mbali ukiwemo wa UVIKO 19.

Akizungumza hatua hizo, Dk. Vendelin Simon kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha ifikapo 2030 jamii inakuwa salama dhidi ya magonjwa yakiwemo ya kuambukizia 

“Kupitia maadhimisho haya tutajiikita zaidi katika kuimarisha mazingira ya usafi katika maeneo ya fukwe na kuyafikia makundi ya wanajamii wakiwemo wanafunzi kwa kuwapatia elimu ya kujikinga na magonjwa na majanga yakiwemo UVIKO 19 kwa kudumisha usafi muda wote,” alieleza Dk. Vendelin.

Nae Amina Kheir, kutoka Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), alisema, wakati dunia inaendelea na mapambano dhidi ya UVIKO 19, UN itaendelea kuimarisha huduma za kinga na tiba hasa ikizingatia kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazopokea wageni kutoka mataifa mbali mbali.

“Sote tunaelewa kwamba kuzuka kwa maradhi haya (UVIKO 19) kumevuruga mifumo ya maisha na kuzalisha changamoto nyingi sio katika mifumo ya afya pekee, bali pia maisha kwa ujumla,” alieleza Amina.

 Afisa Mratibu masuala ya dharua za afya kutoka WHO Zanzibar, Dk. Emma basimaki kutoka WHO, alieleza kuwa ujumbe wa mwaka unaosema ‘Kujijenga tena kwa kuweka mifumo bora ya afya’ umeweka mkazo katika utekelezaji wa lengo la tatu la malengo endelevu ya maendeleo ya dunia (SDGs) linalohimiza kuimarisha afya ya majii.

 Alieleza kuwa ili kukabiliana na changamoto zilizotokana na uviko 19, umoja wa mataifa umedhamiria kuziwezesha serikali kujenga mifumo imara ya kukabiliana na maradhi.

Akieleza mafanikio yaliyopatikana Zanzibar kupitia umoja huo, Ahmed Rashid,  kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), ni pmoja na kufanyika kwa utafiti wa hifadhi ya mtoto mwaka 2009 uliowezesha kutambua athari zinazowapata watoto.

 Alisema utafiti huo ulipelekea kuanzishwa kwa mikakati mbali mbali ikiwemo kuandaa miongozo iliyosaidia kuimarika kwa ulinzi wa motto ikiwemo kuanzishwa kwa madawati jinsia ya jeshi la polisi na sheria ya hifadhi ya motto.

 “Utafiti ule pia uliwezesha kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja wa mwaka 2010 – 2015 ambapo ulianzishwa mpango mpya unaowawezesha wadau kufanya kazi kwa pamoja na kuongezeka kwa ufanisi,” alieleza Rashid. 

 Kwa mujibu ya watendaji hao, umoja wa mataifa kwa kupitia mpango wa kufanya kazi kwa pamoja wa umoja huo, utaendelea kuimarisha mashirikiano na serikali zote mbili za Tanzania kwa kuwajengea uwezo wa kitaaluma, kiufundi na kuzipatia msaada wa vifaa.

 Maadhimisho ya miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania yalianza rasmi Oktoba 23, mwaka huu jijini Dodoma ambapo kilele chake kitafanyika Oktoba 28, mwaka huu jijini Zanzibar ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarjiwa kuwa mgeni rasmi.

Katika kilelel hicho, pamoja na shughuli nyengine, Dk. Mwinyi anatarajiwa kukabidhi zawadi kwa washindi wa andiko la mradi wa ujasiriamali katika maswala ya uchumi wa buluu ambapo jana kulifanyika shughuli za usafi wa mazingira katika fukwe za malindi na upandaji miti kwenye kingo za Mtoupepo.


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango