Wanahabari watakiwa kuzingatia usalama wao wakiwa kazini
NA KHAMISUU ABDALLAH
MJUMBE
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania
(UTPC), Mussa Yussuf, amewataka waandishi wa habari kujiunga na jumuiya za
waandishi ili kuzungumzia changamoto zinazowahusu na kuzipatia ufumbuzi.
Mussa ambae pia ni
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Dodoma alitoa kauli hiyo
wakati akifunga mafunzo ya ulinzi na usalama kwa wanahabari yaliyofanyika jjini
Dodoma.
Alisema ikiwa wanabari
watajiunga na jumuiya hizo, changamoto nyingi zinazowakabili wandishi wa habari
na taaluma ya uandishi wa habari zitapatiwa ufumbuzi na kuleta mabadiliko
katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hata hivyo alikemea
tabia ya makundi ndani ya jumuiya hizo na kueleza kuwa ni adui anaeharibu
jumuiya zao kutofikia malengo waliyojiwekea.
“Tunapokutana
lazima tuzungumze madhaifu yetu kwani moja ya vitu vinavyoharibu jumuiya nyingi
za wanahabari ni makundi na yamejigawa zaidi kimaslahi ni wakati wa kuyasema haya
ili kuzijenga jumuiya zetu,” alibainisha Mwenyekiti Yussuf.
alisema ikiwa wanachama
na viongozi watasimama imara na kuvunja makundi waliyoyaweka ndani ya jumuiya
zao na kuambizana ukweli basi watazijenga jumuiya zao kuwa imara wakati wote.
Akizungumzia suala
la ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, alisema ni jambo la msingi kwa
wanahabari kuweka kipaumbele katika usalama wao binafsi ili kuwa anakuwa salama
wakati wote.
“Usalama wa wanahabari
ukitetereka inayopata hasara zaidi ni jamii ambayo inamtegemea katika kupata
habari hasa za maendeleo ya taifa lao,” alieleza.
Awali akitoa
maelezo ya mafunzo hayo, Afisa Miradi anaeshughulikia mafunzo na machapisho wa
UTPC, Victor Maleko aliwasisitiza wanahabari waliopata mafunzo hayo kueneza
utaalamu huo kwa wenzao ili wengi wanufaike.
Aidha aliwashauri
kutambua mipaka ya kazi zao kwa kufuata misingi ya kazi yao sambamba na kutumia
mbinu mbali mbali wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Jumla ya wanahabari
100 kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania bara na Zanzibar wanatarajiwa kupatiwa
mafunzo ya ulinzi na usalama kupitia mradi huo wa miaka miwili unaotekelezwa
kwa pamoja kati ya UTPC na shirika la International Media Sapport (IMS).
Comments
Post a Comment