Wazazi wekezeni kwenye elimu za watoto wenu - Mbunge
NA MWANDISHI WETU
MBUNGE
wa Jimbo la Dimani, Mustapha Mwinyi Kondo, amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi
wa skuli ya Msingi Kisauni kuwekeza zaidi katika elimu za watoto wao badala ya
mambo mengine yasiyo na tija kwa maisha yao ya sasa na baadae.
Mustapha alieleza hayo wakati wa
sherehe za kuwaaga walimu wa waliostaafu na kuwapongeza wanafunzi waliofaulu
michipuo katika mitihani yao ya taifa ya darasa la sita mwaka 2020.
Katika sherehe hizo zilizofanyika
katika skuli hiyo iliyopo wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, Mbunge huyo alieleza
kufanya hivyo pia kutachangia maendeleo ya skuli hiyo wakati msaada
unapohitajika ili watoto wao kufanya vizuri katika masomo yao.
Alisema licha ya serikali kutoa
elimu bila ya malipo lakini wazazi wanapaswa kuchangia baadhi ya misaada ya
kielimu inapohitajika pale uongozi wa skuli unapowataka wazazi na walezi kutoa
misaada yao katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili Shule hiyo.
Alisema baadhi ya wazazi na walezi
ni wagumu kuchangia maendeleo ya skuli na wapo tayari kugharamika katika
shughuli nyengine za kijamii kama harusi wakati elimu ni msingi wa maisha kwa
watoto wao.
“Baadhi yetu (wazazi na walezi)
wanafanya sherehe za harusi kwa gharama kubwa lakini huwa wagumu kuchangia skuli
kwa ajili ya maendeleo ya watoto wetu huwa wagumu,” alisema Mbunge huyo.
Alisema kuwa walimu wanajukumu
kubwa la kuwasimamia wanafunzi ili kufanya vizuri katika masomo yao na kuwa na
watalamu bingwa hapo baadae.
“Tunafahamu kuwa walimu mna changamoto
nyingi ikiwemo mishahara midogo mnayopata lakini changamoto hiyo isiwe sehemu
ya kutoonesha bidii zenu katika kutoa elimu kwa watoto wetu,” alisema.
Akisoma risala kwa niaba ya Walimu
wenzake, Mwalimu Maryam Masoud, alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana yakiwemo
ya kuongezeka kwa ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi, skuli hiyo inakabiliwa na
upungufu wa madarasa hali inayopelekea msongamano wa wanafunzi madarasani hadi
kufikia wastani wa wanafunzi 120.
Alisema hali hiyo ya wingi wa
wanafunzi madasani linashusha ufanisi katika utendaji kwa Walimu na wanafunzi
wakati darasa moja linahitajika kuwa na wastani wa wanafunzi 45.
Aliitaja changamoto nyengine kuwa ni
uchakavu wa madarasa ambayo baadhi ya madasa yamejaa vumbi kutokana na
kuvunjika kwa saruji iliyowekwa sakafuni jambo ambalo linahatarisha afya za
walimu na wanafunzi.
Kwa upande wake Kaimu Mwalimu Mkuu
wa Skuli hiyo, Ahmada Haji, alisema walimu waliostaafu ni waaandaaji wazuri wa
wanafunzi wa ambao baadhi yao wamefanikiwa kufaulu vizuri mitihani yao ya
taifa.
Mwalimu Ahmada pia aliwapongeza
wanafunzi wa kike kwa kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya taifa mwaka
jana ikilingnaishwa na wanafunzi wa kiume na kuwahimiza wanafunzi wote kusoma
kwa bidii na kuachana na vitendo viovu ambavyo vitawasababishia kutofikia
malengo yao.
Skuli ya Kisauni Msingi iliyoanzishwa
rasmi mwaka 1992 ikiwa na wanafunzi 325 (Wanaume 167 na Wanawake 162) kwa sasa ina
wanafunzi 1,569 ambapo katika kipindi cha mwaka 2013 - 2020 imepasisha
wanafunzi 35 wa mchipuo ambapo wanafunzi watatu wa kike waliofaulu michipuo
mwaka 2020 walitununikiwa zawadi.
Comments
Post a Comment