Puma yawatunza vinara kampeni usalama barabarani
- Ni wanafunzi walioshiriki shindano la michoro
NA MWANDISHI WETU
WADAU
wa usalama barabarani nchini limaetakiwa kuchukua hatua kwa madereva wanaofanya
matumizi yasiyo sahihi ya barabara ili kuona kiwango cha ajali barabarani
kinapungua.
Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud
Mohammed Mussa, aliyasema hayo alipokua akikabidhi zawadi kwa wanafunzi
waliofanya vizuri kwenye zoezi la uchoraji lililoandaliwa kupitia kampeni ya
kupunguza ajali za barabarani, hafla iliyofanyika Skuli ya Kiembesamaki ‘A’, Zanzibar.
Alisema ni vyema kudhibiti matumizi
yasiyo salama kwa madereva wa vyombo vya usafiri barabarani kwa kuona madereva
wote wanafuta sheria na taratibu zilizowekwa.
Mahmoud alisema hatua hiyo lazima iende
sambamba na kufanya udhibiti wa vyombo visivyo fuata utaratibu wa matumizi
sahihi ya barabara ili kuepusha ajali zisiso za lazima.
Alieleza kuwa kikosi cha Polisi wa
Usalama Barabarani kinapaswa kusimamia utekelezaji wa sheria za usalama kikamilifu
kwa kuongeze nguvu katika kudhibiti ajali za barabarani.
Hata hivyo alitaka jeshi hilo
kufanya zoezi la msako maalumu ili kuona madereva wanaoendesha vyombo hivyo
wanakua na leseni zinazotambulika kisharia kwa lengo kuondoa kero za watoto
ambao mara nyingi wanatumia barabara wakati wa kwenda na kurudi skuli.
Aliwaomba wafadhili wa mradi huo
kuendelea kutoa elimu ya kuhamasisha umma juu ya usalama barabarani kwa
watumiaji wa barabara na katika skuli za msingi na sekondari maeneo mbali mbali
ya Unguja na Pemba ili kuona wanafunzi wote wanakua salama sambamba na kufikia
lengo husika la maradi.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar Fatma Rajab alipongeza wadau wa
mradi huo uliokusudia kuondoa hofu jamii ikiwemo walimu na wazazi juu ya sula
zima la ajili kwa wanafunzi.
Katibu huyo aliwapongeza walimu wa
skuli mbali mbali kwa kuibua vipaji vya wanafunzi, hivyo alisema kupitia wizara
hiyo inawajibu wa kuendeleza vipaji vya wanafunzi na kuona wanapata mafanikio na
kunyanyua vipaji vyao.
Kwa upande wake, Meneja wa Mauzo wa rejareja wa Puma Energy Tanzania, Venessy
Chilambo, alisema suala la usalama barabarani limepewa kipaumbele na
kuwekewa mkazo zaidi kutokana na kuonekana limeathiri zaidi wanafunzi ambao
ndio viongozi wa baadae.
Alisema mafunzo hayo yamesaidia
kupunguza ajali kwa wanafunzi ambao ndio tegeo la taifa hili kwa kupata
wanafunzi salama wenye uelewa wa kujikikinga na kujiepusha na ajali zisizo za
lazima kutokana na kupewa elimu hiyo mapema wakiwa maskulini.
Alieleza kuwa takwimu za shirika la
afya ulimwenguni (WHO), zinaonesha zaidi ya watu milioni 1 wanapata ajali
kutokana na matukio mbalimbali yanayosababishwa na vyombo vya usafiri
barabarani hivyo kila mmoja anapaswa kuchukua hatua za kupunguza tatizo hilo.
Alifahamisha zaidi ya wanafunzi
40,000 wamepatiwa mafunzo hayo kwa upande wa skuli za Zanzibar kutokana na
shughuli za kijamii kuongezeka na kuongezeka kiwango cha magari hapa nchini.
Mapema Mkuu wa kituo cha polisi Mazizini,
Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Salum Amir Ngayana, alisema kampeni hiyo
inaenda kuimarisha usalama ambapo kwa kiasi kikubwa itapunguza ajali zisizo za
lazima kwa watoto.
Alisema mara nyingi uzembe wa
madereva wa barabarani ikiwemo suala la kuacha kufuata sheria na alama za
barabarani ndi chanzo cha ajali zinazojitokeza, hivyo alitumia fursa hiyo
kuwataka madereva wote kufuata sheria bila shuruti ili kumaliza suala la ajali
za barabarani.
Nae Meneja wa AMEND Tanzania, Neema
Swai, alisema mradi huo umelenga wanafunzi wa skuli za msingi ili kubadilisha
tabia za matumizi ya barabara wakiwa na umri mdogo hali ambayo itapunguza
tatizo hilo kwa kipindi kinachokuja.
Alisema mafunzo hayo ni chachu ya
watoto wa skuli za msingi kujua namna bora ya kujiepusha na kujikinga na ajali
zisizo za lazima hivyo aliomba jamii kutoa mashirikano zaidi kufanisha jitihada
hizo kama walivyokusudia.
Zoezi la kukabidhi zawadi
limefanyika kwa wanafunzi wa skuli za msingi, Bububu, Mtopepo, Kiembesamaki,
Dole na Fuoni ambapo mshindi wa kwanza alikuwa Khalid Mohammed Said wa Mtopepo,
aliyezawadiwa shilingi 500,000 wakati skuli yake ilipatiwa shilingi Milioni 4
zilizotolewa na Puma Energy Tanzania.
Meya wa Jiji la Zanzibar, Mohamoud Mohamed Mussa(watatu kulia) akikabidhi kikombe kwa mshindi wa Shindano la michoro wa Usalama Barabarani kwa skuli za Msingi Zanzibar lililondaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania kwa kushirikiana na AMEND Africa, Khalid Mohamed Said anayesoma darasa la sita skuli ya Msingi Mtopepo 'B' Zanzibar.
Comments
Post a Comment