Dk. Mwinyi kufungua mkutano wa wataalamu kudhibiti ‘ufisadi’

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (pichani), anatarajiwa kufungua mkutano na mafunzo ya wataalamu wa kudhibiti rushwa na ufisadi nchini Tanzania utakaofanyika baadae wiki hii.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wataalamu wa Kudhibiti rushwa na uhujumu uchumi tawi la Tanzania (ACFE), Msomi Maira, alieleza kuwa mkutano huo utaanza Disemba 13 - 15, mwaka huu katika hoteli ya Madinatul Bahr, Mbweni.

Mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha wataalamu na watendaji wanaohusika na masuala ya udhibiti wa vitendo hivyo vyenye athari za kiuchumi na kijamii.

Msomi aliongeza kuwa lengo la kufanyika kwa mkutano huo sambamba na mafunzo ni kujenga uelewa ili kuongeza idadi ya wataalamu hao lakini pia ufanisi wa taasisi zinazosimamia udhibiti wa ufisadi.

“Wazungumzaji wakuu katika mkutano huo ni pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali (CAG) wa Zanzibar, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mkurugenzi Mkuu wa ZAECA pamoja na wataalamu wa masuala ya fedha, wakaguzi wa ndani na nje wa taasisi za umma na maofisa manunuzi,” alisema Maira.

Aidha maira alipongeza hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya nane katika kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi jambo linaloongeza uwajibikaji katika taasisi za umma na maendeleo kwenye jamii.

Kwa upande wake mwakilishi wa taasisi hiyo upande wa Zanzibar, Mkaguzi Ali Mabrouk Juma, alieleza kuwa udhibiti wa rushwa na ufisadi ni taaluma inayolenga kupunguza vitendo hivyo katika taasisi hivyo ipo haja ya kuwekwa mifumo madhubuti.

“Mkutano huu ni fursa muhimu kwa wataalamu wa masuala ya udhibiti wa Zanzibar kwani mbali ya kujenga uelewa tutapata nafasi ya kuongezeka kwani hadi sasa kuna wadhibiti wachache wanaotambulika,” alieleza Mabrouk.

Aliongeza kuwa iwapo kutakuwa na mifumo imara na yenye kudhibiti vitendo vya rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi, kuna uwezekano wa kupunguza vitendo hivyo kwa zaidi ya asilimia 50 ambapo asilimia tano ya mapato ya serikali ulimwenguni kote hupotea kutokana na vitendo hivyo.

Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2013 na kufanya kazi zake nchini, ni sehemu ya taasisi ya kimataifa inayofanya kazi hizo kwa lengo la kusaidia serikali kuzuia vitendo hivyo kwa kutoa mafunzo na kushirikiana kuandaa sera na miongozo kufanikisha azma hiyo.

PICHA:

MTENDAJI Mkuu wa taasisi ya Taasisi ya Wataalamu wa Kudhibiti rushwa na uhujumu uchumi tawi la Tanzania (ACFE), Msomi Maira (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mkutano na mafunzo kwa wadau wa taasisi hiyo utakaofanyika kuanzia Disemba 13 - 15, 2021, Zanzibar.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango