Hai yatumia fedha za UVIKO 19 kujenga madarasa 43

NA MWANDISHI WETU, HAI

MPANGO wa maendeleo kwa ustawi na mapambano dhidi ya UVIKO - 19, umefanikisha ujenzi wa vyumba 43 vya madarasa katika skuli ya sekondari uliogharimu shilingi milioni 860 katika wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Mkuu wa wilaya hiyo Hai, Juma Irando (pichani) aliyasema hayo hivi karibuni katika taarifa yake kwa Kamati ya Siasa mkoa wa Kilimanjaro iliyongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Patrick Boisafi walipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM na mapambano dhidi ya UVIKO – 19 wananchi 28,877,019 wamepatiwa chanjo ya ugonjwa huo.

Irando alisema ujenzi wa madarasa hayo utakamilika kabla ya Disemba 31 mwaka huu na wanafunzi 3,950 wakiwemo wasichana 2,050 na wavulana 1,900 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa kipindi cha Januari mwakani wataanza masomo yao kama serikali ilivyoagiza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM mkoa huo,  Patrick Boisafi, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuhakikisha tatizo la uhaba wa wa vyumba vya madarasa na msongamano wa wanafunzi linakwisha mashuleni.

Aidha aliwapongeza Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na wananchi kwa kushirikiana kwa hali na mali na serikali kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo kwa ubora wa hali ya juu na muda uliopangwa.

Boisafi alisema hatua hiyo itahakikisha wanafunzi wote watakaochaguliwa wanaanza masomo yao Januari mwakani wakikuta madaraa na samani zikiwa tayari.

"Rais Samia Suluhu Hassan amefanikisha kupatikana kwa shilingi tirioni 1.3 za ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa nchi nzima ili kuondokana na tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa na masongamano wa wanafunzi madarasani,"alisema Boisafi.

Katika hatua nyingine Boisafi, alizishauri Halmashauri za Wilaya na Manispaa kuanza utamaduni wa kutenga fedha katika akaunti maalumu kwa ajili ya kufanyia ukarabati majengo ya serikali yanapochakaa, ikiwemo majengo ya shule, hospital, zahanati na vituo vya afya.

“Huko nyuma kulikuwa na utaratibu wa kutenga fedha za ukarabati wa majengo ya serikali kuanzia yalipojengwa na kwamba utaratibu huo ulikuwa mzuri, hivyo Kamati ya Siasa ya mkoa inazielekeza  halmashauri zote kuhakikisha zinatenga fungu la fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya serikali,” alieleza Mwenyekiti huyo.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa, Selemani Mfinanga, alisema CCM mkoani Kilimanjaro ina kila sababu ya kuwapongeza Walimu Wakuu, Maofisa elimu, kamati za ujenzi kwa kushirikiana na wananchi kwa kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo kwa ubora unaotakiwa licha ya kuwapo kwa changamoto mbali mbali.

Mpango wa maendeleo kwa ustawi na mapambano dhidi ya UVIKO - 19, ulizinduliwa  na rais samia suluhu Hassan, mwezi oktoba mwaka huu ukilenga kutumia fedha za mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kutoka shirika la fedha ulimwenguni (IMF) katika maeneo mbali mbali ili kuleta nafuu ya athari za ugonjwa huo.

 

Miongoni mwa maeneo ya utekelezaji wa mpango huo ni pamoja na ununuzi magari ya wagonjwa ya kisasa 20 na magari ya kawaida 365, ujenzi wa vituo vya dharura na vifaa kwa hospitali za taifa hadi halmashauri, uimarishwaji wa mfumo wa usambazaji na ununuzi wa mitungi ya gesi katika hospitali za rufaa na utekelezaji miradi ya elimu kama vile madawati, vyumba vya madarasa katika vyuo 17.


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango