ZATUC yahimiza wafanyakazi kutambua sheria za kazi, ajira
NA MWANDISHI WETU
SHIRIKISHO
la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), imesema kuna umuhimu kwa wafanyakazi
kujua sheria za kazi ili ziweze kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao
pamoja na kuwaongoza pale wanapotaka kudai haki zao.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Khamis
Mwinyi Mohammed (pichani), alisema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika kikao
cha kujadili haki za wafanyakazi na utekelezaji wake kilichoandaliwa na Shirika
la msaada la kimataifa la Actionaid katika ukumbi Kitengo cha kudhibiti Malaria,
Mwanakwerekwe.
Alisema asilimia kubwa ya
wafanyakazi hawajui sheria hizo jambo ambalo husababisha kuleta mkanganyiko
mkubwa baina yao na waajiri pale kunapobidi kudai baadhi ya haki zao.
“Wafanyakazi wanakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo upataji wa haki zao, kwani asilimia kubwa wanashindwa
kutofautisha haki za msingi na nyenginezo jambo ambalo husababisha kuleta
malalamiko ndani ya taasisi mbalimbali,” alisema.
Sambamba na hayo alisema kutokana
na hali hiyo wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuwapatia elimu
wafanyakazi hao ili waweze kufahamu sheria hizo na kuzifanyia kazi ili kuona
kila mfanyakazi ananufaika nazo.
Aidha Mwinyi alitumia fursa hiyo
kuzitaka taasisi mbali mbali kuona umuhimu wa kuwapatia taaluma wafanyakazi wao
ili kila mmoja aweze kuzifanyia kazi.
Kwa upande wa Mratibu wa shirika la
Actionaid, Baker Khamis, alisema wameamua kutoa mafunzo hayo ili kuondosha
baadhi ya changamoto zinazowakwaza wafanyakazi kutokana na kutofahamu sheria za
kazi.
Alisema wataendelea kutoa elimu
hiyo kwa wafanyakazi wa kada mbalimbali ili ziweze kuwasaidia katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema wafanyakazi wanakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo taratibu za mikataba hazifuatwi, mishahara midogo na
mambo nyengine hivyo kupitia mafunzo hayo yatasaidia kuweza kufahamu sheria
izo.
Kwa upande wa washiriki wa mkutano
huo walisema wafanyakazi wengi wanazikosa haki zao makazini mwao kwa kuwa
hawajui sheria na hatua za kufuata ili waweze kupata haki hizo.
Miongoni mwa washiriki hao Haji
Maktuba Haji, kutoka taasisi ya watembeza watalii alisema kuna mahitaji makubwa
ya kutolewa elimu hiyo kwa wafanyakazi ili kuwaondoshea changamoto mbali mbali
wanazokuta nazo.
“Tumekuwa tukikutana na changamoto
mbali mbali ikiwemo ya upatikanaji wa haki kutokana na wengi wetu kushindwa
kufuatia sheria na taratibu zilizowekwa,” alieleza Haji.
Kwa upande wa mwanasheria Jambia
Jambia, ambae aliyekuwa mkufunzi wa mafunzo hayo, alisema sheria za kazi zimetungwa
ili kusaidia kila mmoja kufahamu wajibu na majukumu yake pamoja na kuondosha
migogoro ndani ya sehemu za kazi.
Mafunzo hayo ya siku moja
yamewashirikisha wafanyakazi kutoka taasisi mbali mbali za serikali na binafsi
yaliandaliwa na Actionaid kwa lengo la kujenga uelewa na uwezo wa wafanyakazi
kuzitambua sheria za kazi na ajira.
|
|
Comments
Post a Comment