Andikeni
habari zitakazotatua migogoro – Mfaume
KHAMISUU
ABDALLAH NA MADINA ISSA
WAANDISHI
wa habari nchini wameshauriwa kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro ili kuifanya
jamii kuwa na mshikamano utakaosaidia kuondoa tofauti hasa za kisiasa na kuharakisha
maendeleo ya nchi.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa
Habari Zanzibar (ZPC), Abdalla Abdulrahman Mfaume, alieleza hayo jana wakati
akifungua mafunzo ya uandishi wa habari za utatuzi wa migogoro na ujenzi wa
amani kwa wanahabari wa vyombo mbali mbali yaliyofanyika katika ukumbi wa Kitengo
cha Uzazi Shirikishi, Kidogochekundu Mjini Unguja.
Alisema kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa, mara nyingi
waandishi wa habari hujikita zaidi katika uandishi wa habari za siasa kipindi
cha uchaguzi tu hali inayochangia uwepo wa migogoro hiyo.
“Ikiwa tutaripoti na viongozi wakasikia
basi migogoro mingi iliyopo katika jamii inaweza kufuatiliwa na kutatuliwa na
hili ndio lengo letu la kutoa mafunzo haya,” alibainisha.
Akizungumzia lengo la mafunzo hayo alisema
ni kuhakikisha waaandishi wa habari, wanajengewa uwezo juu ya uandishi wa habari
zitakazozuia na kutatua migogoro.
Mapema Katibu wa ZPC, Mwinyinvua Abdi Nzukwi, alisema mafunzo
hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa jenga amani yetu unaotekelezwa kwa pamoja
na Search for Common Ground, Kituo cha huduma za sheria Zanzibar (ZLSC) na
Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
“Mafunzo haya yana manufaa makubwa
kwao na yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika majukumu yao ya kila siku hivyo
ni vyema wakazingatia ili kuongeza weledi na maarifa yatakayosaidia kudhibiti
na kutatua migogoro badala ya kuchochea,” alieleza Nzukwi.
Akiwasilisha mada ya dhana na
vyanzo vya migogoro, Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Ali Haji Mwadini, alisema kuna
migogoro mbali mbali katika jamii, familia na sehemu za kazi inayosababishwa na
uchache wa rasilimali, pesa, madaraka, ajira, makundi yenye dhana potofu.
“GNU (Serikali ya Umoja wa Kitaifa)
ina manufaa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar, hivyo vyombo vya habari vina
jukumu la kuhakikisha umoja, mshikamano na maelewano yaliyopo yanaendelezwa,”
alisema Mwadini ambae pia ni mhariri mtendaji wa shirika la magazeti ya
serikali Zanzibar.
Hivyo, alibainisha kwamba ni vyema
kwa wanahabari kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa serikali hiyo
ambayo imetokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na vyma vya CCM na ACT -
Wazalendo.
Baadhi ya wanahabari walioshiriki
mafunzo hayo walisema, yana umuhimu mkubwa kwao katika kuelimisha na kuibua
changamoto zinazoikabili jamii na kuelimisha umuhimu wa serikali ya umoja wa
kitaifa ambayo ina manufaa makubwa katika taifa.
Bakari Masoud kutoka Plus Radio na
Amina Mchezo wa Coconut FM, walisema wanahabari wana nafasi kubwa katika
kuisaidia jamii kutatua migogoro na kuona jamii inafaidika kupitia uwepo wao.
Aidha walisema wanahabari ni daraja
kutoka sehemu moja kwenda nyengine kwa kuwasemea wananchi ambao sauti zao ni
ndogo na kuweza kufanyiwa kazi hivyo ni jukumu lao kutumia kalamu zao,sauti zao
na vyombo vyao katika kutatua migogoro hiyo.
Walimpongeza muwezeshaji huyo kwa
kuwakumbusha jukumu lao katika jamii katika kutatua migogoro mbalimbali ili
kuona Zanzibar inaendelea kuwa na amani umoja na mshikamano na nchi inapiga
hatua kiuchumi.
Mafuzo hayo ya siku tatu
yameandaliwa ZPC kupitia mradi wa Jenga Amani Yetu unaotekelezwa na Search for
Common Ground, Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLCS) na Kituo cha Msaada
wa Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) yamefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).
Comments
Post a Comment