NMB, Mambo ya kale wakubaliana kuimarisha utalii Zanzibar
NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar imetiliana saini makubaliano ya kuimarisha shughuli za watembeza watalii na benki ya NMB kwa kutoa mafunzo ili kurasimisha shughuli zao waweze kukopesheka.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma Mabrouk Khamis, alitia saini kwa niaba ya wizara hiyo huku Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi Filbert Mponzi aliiwakilisha benki ya NMB.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Fatma alisema benki makubaliano hayo yamelenga kuinua shughuli za vijana wanaotembeza watalii nchini.
Alieleza kuwa mitaani kuna vijana wengi wanaofanya kazi ya kuongoza watalii bila ya
ujuzi wa kutosha hivyo kuharibu taswira ya Zanaibar hivyo makakati huo utawasaidia
kuimarishawa ujuzi na maarifa yao.
“Wapo vijana
wanaojihusisha na utalii mfano ‘beach boys’ ambao wanafanya utalii wa mikobani
na mara nyingi wanakuwa kero kwa wageni. Kupitia makubaliano haya, tutawapa
mafunzo na kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kuwarasimisha na kuwaongoza,”
alisema Fatma.
Mbali na hayo
alibainisha kuwa wizara ina mpango wa kuimarisha mashamba ya viungo, ambayo
yanatumika na vijana wanaojihusisha na shughuli hizo.
“Tutashirikiana
kuwapa mafunzo na mikopo kuimarisha bidhaa zao, tutawashika mkono ili
kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na bidhaa nzuri,” alisema Fatma.
Alieleza kuwa
katika ziara waliyofanya hivi karibuni, wamebainoi kuwa yapo mashamba ya viungo
yasiyo na viwango hivyo wizara ina mkakati wa kuanza kuhuisha vijiji ili kuwa
na vijiji vya utalii.
Nae Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, alisema benki
hiyo imefanya mambo mengi visiwani Zanzibar kwa lengo la kuinua sekta ya
utalii.
Alieleza kuwa
katika kuendeleza azma hiyo, wameamua kupeleka vituo vya mauzo 100 na kuiomba
Wizara ya Utalii kuwaelekeza vituo watakaposambaza vifaa kwa ajili ya kufanyia
malipo.
“NMB ndio benki kubwa zaidi nchini ambayo serikali ni mdau mkubwa lakini pia inaongoza kwa kupata faida yaani kwa ukubwa, tunapoingia kwenye jukumu kama hili hatuna wasiwasi,” alisema Mponzi.
“Tumeamua
kujifunga kwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar maana yake tutafanya
kitu kikubwa katika utalii Zanzibar,” alisema Mponzi.
Mponzi alisema
kufanya hivyo ni kuunga mkono safari ya kuimarisha uchumi wa bluu na kwenda
sambasamba na dunia ili kukuza uchumi kupitia mifumo ya kidigitali katika
shughuli za utalii nchini.
Alisema hatua
hiyo inalenga kutoa elimu na kuhamasisha watalii wazidi kutembelea vivutio vya
kitalii vilivyopo Zanzibar kupitia matamasha na promosheni mbali mbali.
Aliongeza kuwa
watasambaza mashine za malipo kwenye vituo vya makusanyo na vivutio vya utalii
ili kuwawezesha watalii kulipia ada na tozo zote kupitia kadi zao za
kielektroniki za Mastercard, Visa na UnionPay.
Alifafanua
kuwa hatua hiyo itapunguza ulazima wa watalii kutembea na fedha
taslim hivyo kuwawezesha kufanya malipo kwa njia salama na rahisi.
Comments
Post a Comment