Mtoni Kidatu wahimizwa kulinda maeneo ya skuli

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Suzan Peter Kunambi, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanalinda rasilimali ya ardhi ya elimu ili kuona hayavamiwi kiholela.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizugumza na wananchi wa Mtoni Kidatu alipokuwa akisikiliza changamoto zinazowakabili walimu wa skuli ya Mtoni Kidato. 

Alisema kuna uvamizi mkubwa katika maeneo ya skuli zilizomo ndani ya wilaya yake kutokana na wananchi kujenga makaazi ya kudumu.

“Sio skuli hii tu iliyovamiwa, skuli vinazovamiwa ni nyingi hivyo ni wajibu wa wananchi mliopo karibu na maeneo ya skuli mnapoanza ujenzi msikae kimpya kwani mipaka ya skuli inajulikana na kuwasisitiza walimu kuacha kuazima maeneo ya skuli,” alisisitiza.

Alisema ni vyema kuwa walinzi wa maeneo hayo kwani bado yana shughuli kubwa kwani bado miundombinu ya elimu inahitajika kujengwa ya kisasa.

Aidha alisema maeneo mengi yanavamiwa na pale serikali inapotaka kujenga majengo ya horofa ya skuli inakuwa na changamoto kubwa ya kukosa maeneo kutokana na maeneo mengi kuvamiwa.

“Haya ndio yanayotukuta sasa hivi, wizara imepanga kutujengea skuli ya ghorofa katika eneo la Mtopepo hatuna eneo kwani eneo lote limevamiwa sasa niwaombe eneo hili ambalo bado lipo kidogo basi ni sote tulilinde,” alisisitiza Kunambi. 

Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Haidar Yahya Issa, alisema skuli yao inakabiliwa na changamoto kubwa wa uvamizi wa maeneo yao  kwa maakazi ya nyumba hali ambayo inatokana na kukosa kwa hatimiliki ya eneo lao. 

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amal,  Ali Khamis Juma, alisema ni kweli maeneo mengi ya skuli yamekuwa yakivamiwa kwa maakazi hivyo aliziomba ofisi za wilaya, shehia na kamati za skuli kuhakikisha wanasaidia kutovamiwa kwa maeneo ya skuli.

Aidha Katibu Ali alisema serikali na wafadhili wengine zinajitahidi kuongeza miundombinu nzuri katika skuli zake lakini wapo watu wachache wanaona mambo hayo sio muhimu hivyo ni vyema kudhibitiwa watu hao kwa nguvu zote.

Mwalishi wa Jimbo la Mwera, Mihayo Juma N’gunga ni alikiri baadhi ya wananchi kujimilikisha baadhi ya maeneo ya skuli kwa ujenzi wa nyumba za makaazi hasa katika skuli zote zilizokuwepo ndani ya jimbo hilo.

Aliyataja maeneo hayo alisema ni pamoja na skuli ya Mtoni Kidatu, Regezamwendo, Kianga, skuli ya Chunga changamoto ambayo ipo kwa asilimia kubwa katika Mkoa huo.

Aliahidi kuwa kwa kushirikiana na serikali ya wilaya na mkoa wanategeneza utaratibu maalum kwa watu wote wanaovamia na kuhakikisha skuli zote zilizokuwepo ndani ya jimbo hilo zinapata hati za maeneo yao ili kuweza kulinda mipaka yake.

Alisema kuvamiwa kwa maeneo mengi ya skuli kunatokana na kukosekana kwa hatimiliki jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi kwa nguvu zote.

Alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya skuli ili kuweza kusaidia ujenzi pale serikali inapotaka kuongeza madarasa kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanapata elimu katika maeneo ya karibu.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango