Polisi, wanahabari wakubaliana kushirikiana
NA
MWANDISHI WETU
WAANDISHI wa habari na watendaji wa jeshi la polisi wameahidi kuendelea kushirikiana katika utendaji wa kazi zao kwa maslahi ya taifa.
Makubaliano
hayo yalifikiwa katika mdahalo wa kitaaluma ulioyakutanisha makundi mawili hayo
na kujadili wajibu na majukumu yao.
Mdahalo huo
uliokuwa na maudhui ya usalama kwa waandishi wa habari na mahusiano kati ya
waandishi wa Habari na jeshi la polisi, yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa
Habari Zanzibar (ZPC) kupitia mradi wa
usalama kwa wandishi wa habari unaotekelezwa na muungano wa klabu za waandishi
wa Habari Tanzania (UTPC) na Shirika la International Media Support (IMS).
Akifungua mdahalo
huo uliofanyika katika jengo la ZURA mjini Unguja, Mwenyekiti wa ZPC, Abdalla
Adulrahman Mfaume, alisema jeshi la polisi lina wajibu wa kuhakikisha waandishi
wa habari wanafanya kazi katika mazingira salama na kuhakikishiwa ulinzi.
Hata hivyo,
alisema wakati mwengine hujitokeza changamoto zinazosababisha pande hizo mbili
kutoaminiana hali inayopaswa kuondoka.
Licha ya
changamoto hizo, alisema bado pande hizo mbili zinaendelea kushirikiana
kuhakikisha jamii inapata taarifa stahiki na kwa wakati.
Akizingumza
kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi, mkuu wa utawala wa jeshi la polisi mkoani
humo, Kamishna Msaidizi wa Polisi,
Abubakar Khatib Ally, alisema mkutano huo ni fursa muhimu kwa waandishi
wa habari na polisi kushirikiana na kujenga uhusiano mwema katika kazi zao.
Alisema
licha ya tofauti zinazojitokeza bado pande hizo mbili zinahitaji kufanya kazi
kwa pamoja katika kutoa taarifa kwa wananchi.
Hata hivyo,
aliiomba ZPC kutumia mafunzo yanayoandaliwa na jeshi la polisi kwa askari wake
kutoa mada kuhusu uhusiano mwema wa waandishi na jeshi la polisi ili ushirikiano
uliopo uendelee.
Aidha
wakiwasilisha mada kwenye mdahalo huo, Mwandishi mwandamizi wa habari, Dk.
Saleh Yussuf Mnemo na ASP Ramadhan Himid Haji kutoka makao makuu ya polisi
Zanzibar, walisisitiza umuhimu wa pande mbili hizo kushirikiana na kuvumiliana katika utendaji kazi wa pande
hizo mbili.
Walieleza
kuwa licha ya kila taaluma kuwa na misingi yake, bado makundi hayo
yanategemeana katika kukamilisha majukumu yao hivyo ipo haja ya kushirikiana
kikamilifu.
Aidha waliiponeza waandaaji wa mdahalo huo kwa kutoa fursa wa watendaji wa pande zote mbili kujadili kwa pamoja changamoto na mafanikio yaliyopo hatua ambayo itasaidia kufikia malengo ya kuwa na Tanzania yenye amnani, utulivu na Uhuru wa kujieleza.
Comments
Post a Comment