ZBS yatekeleza agizo la Dk. Mwinyi kuwezesha wajasiriamali

NA MWANDISHI WETU

WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kuzingatia ushauri na maelekezo yanayotolewa na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) ili kuimarisha uzalishaji na kuyafikia masoko.

Wito huo umetolewa na mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Yussuf Majid Nassor, katika hafla ya utoaji vyeti vya ithibati ubora kwa wajasiriamali, iliyofanyika katika ofisi za taasisi hiyo Amani, mjini Unguja.

Alieleza kuwa mchakato wa ukaguzi na kuwathibitisha wajasiriamali hao ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyezitaka taasisi zinazohusika na wajasiriamali kuwasaidia na kuwaendeleza ili kukuza ajira nchini.

Alieleza kuwa kabla ya hatua hiyo, wajasiriamali kutoka vikundi 10 walipatiwa mafunzo na kufuatiliwa kuelekezwa namna ya kuzalisha bidhaa zenye ubora ambapo vikundi vinne vimekamilisha hatua zote na kupatiwa alama ya ubora ya ZBS.

“Hawa sita waliobakia bado tunaendelea kukamilisha hatua za kuimarisha maeneo yao ya uzalishaji na tunaamini kabla ya kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha watakuwa wamefikia viwango,” alieleza Yussuf.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha uangalizi, mbali ya mafunzo ya kuwajengea uwezo, pia gharama za ukaguzi wa bidhaa zimepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 90 ambapo aina moja ya bidhaa imelipiwa shilingi 50,000.

“Awali ili mtu afikie hatua ya kupatiwa cheti cha alama ya ubora, alitakiwa kulipa kati ya shilingi 720,000 na milioni moja lakini kupitia mpango huu, mjasiriamali analipa shilingi 50,000 pekee ili kuwahamasisha lakini pia kuwaendeleza,” aliongeza.

Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho, mjasiriamali mzalishaji wa vipodozi asilia kutoka Zaydat Product, Tatu Suleiman, alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuuza bidhaa zao katika masoko ya nje ya Zanzibar.

Naye mwakilishi wa kampuni ya Bedi Interprise ya Bopwe Wete Pemba, Ashura Khalifa Hamad, alieleza kuwa mchakato wa kufikia kupata cheti cha ubora umewaimarisha na kuishukuru serikali kupitia ZBS na SMIDA kwa kuwajengea uwezo.

Naye mwakilishi wa Mtule Amcos, mwalimu Khamis Seif Ali aliwahimiza wajasiriamali wenzake kufuata miongozo inayotolewa na taasisi hizo ili kuyafikia masoko ya ndani na nje na kwenye sekta ya utalii.

Aliongeza kuwa kufuatia hatua hiyo wamedhamiria kuanza usindikaji wa mazao ya ndimu pamoja na kuzalisha ‘tomato paste’ pamoja na ‘tomato paste’ wanayozalisha hivi sasa.

Vikundi vilivyopatiwa alama ya ubora ya ZBS katika hafla hiyo ni Zaydat Product, Mtule Amcos, Victory Group na Bedi Enterprises wakati vikundi vya Tushikamane Partnership, jukumu, SiPekeYangu Enterprises, Zanop, Ultrafine Products na Bopwe Vegetable & products vikiendelea na mchakato.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango