KILELE SIKU YA VIWANGO AFRIKA

Uzalishaji, usafirishaji bidhaa uzingatie viwango kulinda afya

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, ameeleza kuwa katika kushajihisha ukuaji wa biashara, uzalishaji, uagiziaji na usafirishaji bidhaa unapaswa kuzingatia viwango na ubora vilivyowekwa.

Alieleza hayo jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mtendaji wa Baraza la Leseni Zanzibar, Rashid Ali Salim, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya viwango Afrika iliyoadhimishwa ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein katika jengo la mamlaka ya udhibiti wa maji na nishati Zanzibar (ZURA).

Alieleza kuwa bidhaa zenye viwango, zinazokubalika katika biashara za kimataifa kwani zina uhakika wa kulinda afya za watumiaji na mazingira.

Alieleza kuwa utumiaji wa bidhaa zilizo chini ya kiwango hupelekea athari nyingi zikiwemo za kimazingira na kuzagaa ovyo kwa takataka zinazotokana na bidhaa hizo.

Aidha aliwakumbusha viongozi na watendaji wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) kufanyakazi kwa bidii, ubunifu, uaminifu na kujiamini zaidi katika kusimamia majukumu waliyopewa kwa mujibu wa sheria.

Waziri huyo pia aliwataka wafanyabiashara kushirikiana kikamilifu na ZBS ili kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa nchini zinakidhi matakwa ya viwango kulinda afya na usalama wa watumiaji.

Akizungumzia maadhimisho hayo, mkurugenzi mkuu wa ZBS, Yusuph Majid Nassor, alieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiadhimisha siku hiyo kwa mashindano ya insha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Alieleza kuwa hatua hiyo inakusudia kujenga uelewa wa jamii juu ya viwango kulingana na maudhui yaliyopangwa na Shirika la Viwango Afrika (ARSO).

“ZBS (Taasisi ya viwango Zanzibar) ni mwanachama mwangalizi wa ARSO na kwa miaka minne sasa tumekuwa tukishiriki katika mashindano ya insha ambazo huwa na ujumbe wa kuhamasisha matumizi ya viwango,” alieleza Yussuph.

Akiwasilisha taarifa kuhusu shindano la insha kwa mwaka huu, Mkurugenzi Idara ya viwango wa ZBS, alisema jumla ya washiriki 52 kutoka vyuo 14 waliwasilisha kazi zao na kupatikana washindi watano.

Hafsa alieleza kuwa maudhui ya insha hizo ni ‘Jukumu la viwango katika kutatua na kubaini masuala ya kiuchumi na kijamii kwa wahamiaji, wanaorejea majumbani kutafuta ufumbuzi kwa uhamaji wa kulazimishwa barani Afrika’.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya ZBS, Mwanaisha Abdallah Saleh, aliwapongeza washiriki wa shindano hilo na kuwaomba kuwa mabalozi wa kutangaza umuhimu wa viwango kwa maisha ya wananchi na mazingira.

Washindi watatu wa juu wa shindano hilo, makala zao zitashindanishwa na wawakilishi wa nchi nyengine kupata mshindi wa kanda ya Afrika atakaetangazwa katika mkutano mkuu wa shirika la viwango Afrika (ARSO) ambapo katika mwaka uliopita Zanzibar ilishika nafasi ya saba kanda ya Afrika.

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Leseni Zanzibar, Rashid Ali Salim (wa pili kulia) akikabidhi kwa niaba ya Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, mshindi wa kwanza wa shindano la insha kuhusu viwango barani Afrika Maryam Rajab Athuman lililoandaliwa na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS). Kulia ni Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa ZBS, Mwanaisha Abdallah Saleh na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yusuph Majid Nassor

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Leseni Zanzibar, Rashid Ali Salim (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa shindano la insha kuhusu viwango barani Afrika lililoandaliwa na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS). Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa ZBS, Mwanaisha Abdallah Saleh na kushoto ni mkurugenzi wa ZBS, Yusuph Majid Nassor. (PICHA NA MWINYIMVUA NZUKWI).


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango