Watendaji OMKR wakiwa kuongeza ubunifu
NA RAYA HAMAD, OMKR
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya Salum (katikati), amewataka Watendaji wa Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar kuendelea kuwa wabunifu ili kwenda sambamba
na maono ya Serikali ya awamu ya nane ya kutimiza matarajio ya kuwatumikia
vyema wananchi.
Dkt. Mkuya ameyasema hayo wakati wa
makabidhiano ya ofisi baina yake na Waziri mpya wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais, Harous Said Suleiman kufuatia mabadiliko ya baraza la Mapinduzi yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi hivi karibuni.
Amesema kwamba wananchi
wanamatarajio makubwa ya Serikali ya awamu ya nane katika utekelezaji wa sera
na mipango mbali mbali ya maendeleo na kwamba ni vyema wafanyakazi kujitahidi
kwenda sambamba na matarajio hayo.
Hata hivyo, Dkt Saada amewakumbusha
watendaji hao pia kujitahidi kuenda na muda kwa kuzingatia wakati katika utekelezaji wa shughuli za kazi mbali
mbali ili kumsaidia waziri Harusi kutimiza vyema majukumu yake.
Amehimiza wafanyakazi hao kumpa
mashirikiano Waziri Harusi kama walivyompa yeye ili aweze kutumiza majukumu
yake kwa wepesi na kuweza kupata mafanikio katika sekta zote mtambuka
anazoziongoza ndani ya wizara hiyo.
Naye waziri mpya wa Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman, amewaomba wafanyakazi hao kumpa
mashirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais na ujenzi wa nchi kwa jumla.
Amewakumbusha watendaji hao umuhimu
wa kuendelea kufanyakazi kwa mashirikiano na kuheshimu sheria na taratibu za
kazi kama msingi wa mafanikio kazini.
Aidha Harusi amezitaka taasisi zote
za ndani kuhakikisha kwamba zinatayarisha na kutekeleza mpango mkakati katika
utekelezaji wa malengo ya taasizi husika.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak, amemshukuru waziri aliyeondoka Mhe. Dkt Saada
Mkuya kwa usimamizi bora kwa kipindi chote alichokuwepo kwa kutumia umahiri na
maono mapana katika kusimamia sekta zilizopo ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Dkt. Shajak amesema kwamba katika
kipindi kifupi alichoiingoza Ofisi hiyo usimamizi wake umeleta ufanisi kwa
kutekeleza mambo mengi likiwemo suala la mabadiliko ya sheria ya kupambana na
dawa za kulevya Zanzibar.
Makabidhiano hayo yamefanyika
kwenye ukumbi wa mkutano wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani, Zanzibar.
Comments
Post a Comment