Andikeni habari zinazochochea ulipaji kodi kwa hiyari – ZRB

NA MWANDISHI MAALUM

KAMISHNA wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Yussuf Juma Mwenda (pichani), ameviomba vyombo vya habari kuandika habari zinazochocheo ulipaji kodi kwa hiyari.

Mwenda alitoa rai hiyo alipokutana na baadhi ya wajumbe wa kamati ya maandalizi ya tunzo za umahiri wa uandishi wa habari Zanzibar (EJAZ) na maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani (WPFD), ofisini kwake Mazizini Unguja.

Alieleza kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na vyombo vya habari kuelimisha jamii, mkazo zaidi unapaswa kuwekwa kwenye kuhamasisha matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki ili kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji wa kodi za serikali na biashara nchini.

Aliongeza kuwa waandishi wa habari pia wanaweza kuandika habari zitakazoonesha umuhimu na faida ya kodi kwa wananchi ili wawe na utamaduni wa kudai na kutoa risiti wanapofanya mauziano.

"Tungependa kupitia habari zenu mtushauri namna gani tunaweza kuifanya ZBR ikawa ni 'most efficency tax board in Africa' na namna gani Zanzibar itaongeza mapato ya kodi lakini pia kuibua vyanzo vipya," alieleza Mwenda.

Wajumbe wa Kamati hiyo, Salma Said na Farouk Karim mbali ya kumpongeza Kamishna huyo kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo, walieleza kuwa waandishi wa habari kupitia jumuiya zao, wanathamini mchango wa taasisi hiyo katika kukuza uchumi wa Zanzibar na watu wake.

Aidha wajumbe hao walimuahidi Kamishna huyo kwamba, wataendelea kuhamasisha jamii kupitia vyombo vya habari kulipa kodi kwa hiyari sambamba na kujengeana uwezo ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

"Tumekua tukishirikiana na taasisi yako kwa muda mrefu lakini tunataka kukuhakikishia kwamba tutaendelea kufanya hivyo kwa kutambua ukubwa na umuhimu wa kazi mnayoifanya kwa maslahi ya nchi yetu," alisema Karim ambae ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Ziara ya wajumbe hao ni sehemu ya maandalizi ya tunzo na maadhimisho hayo yatakayofanyika mwezi ujao ambapo jana (Aprili 12, 2022) mchana Makamu Mwenyekiti wa Kamati Dk.  Mzuri Issa,  aliongoza kikao kilichojadili maswala mbali mbali ya kufanikisha shughuli hizo.

Kamati inayoratibu shughuli hizo inaundwa na wajumbe kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar), Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kupitia Idara ya mafunzo ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango