Majaliwa: Zingatieni weledi, maadili ya vyombo vya habari

LINDI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ili kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi vyombo vya habari havina budi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi pamoja na kutanguliza uzalendo na maslahi ya taifa.

Pia, Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kusimamia matumizi ya mitandao ya kijamii ili pamoja na kuongeza upatikanaji wa habari kuwepo na uzingatiaji wa maadili na weledi. “Ni matarajio yetu kuwa moja ya majukumu yenu ni kulisemea Taifa letu.” 

Ameyasema hayo Aprili 14, 2022 wakati akizindua vituo vya kurushia matangazo ya redio vya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wilayani Ruangwa, mkoani Lindi kwa niaba ya vituo vingine vya wilaya za Ludewa (Njombe), Mlimba (Morogoro) na Ngara (Kagera).

Amesema SERIKALI itahakikisha uhuru wa vyombo vya habari nchini unaimarishwa na kulindwa hivyo wamiliki na wanahabari wanatakiwa kuzingatia maadili ya kazi zao ili wananchi waendelee kupata taarifa sahihi, kwa urahisi zaidi na kwa wakati.

Waziri Mkuu amewasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari wahakikishe wanahabari wanapatiwa mikataba ya ajira inayozingatia sheria za ajira sambamba na kufanya utafiti wa habari ili kuepuka upotoshaji kwa kuchapisha au kutangaza taarifa zinazolenga kuchonganisha jamii.

Amesema ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata habari mbali mbali zikiwemo za burudani, vituo vya televisheni na redio vinatakiwa kuacha tabia za ubaguzi katika kurusha matangazo hususan kazi za sanaa.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza TBC na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kutekeleza jukumu hili kwa vitendo.”

Amesema Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano  (2020/2021 - 2025/2026) umeweka vipaumbele vyake katika uwekezaji wa miundombinu ya utangazaji ya TBC, ikiwemo upanuzi wa usikivu wa redio, pamoja na miundombinu.

“Kadhalika, Ibara ya 125 ya ilani ya uchaguzi ya CCM inaielekeza serikali kuwekeza katika uimarishaji wa miundombinu ya utangazaji kwa TBC. Hivyo, kuzinduliwa kwa matangazo ya Redio katika vituo vya Ruangwa, Ludewa, Kilombero (Mlimba), Ngara na maeneo ya jirani ni utekelezaji wa ahadi za CCM kwa wananchi kwa kipindi cha 2020 hadi 2025,” ameeleza Majalliwa.

Waziri Mkuu pia amezielekeza TBC, UCSAF na TANESCO kukaa pamoja na kuhakikisha wanatatua changamoto zinazokabili baadhi ya vituo kama vile Ludewa, Mbinga na Kisaki kwa lengo la kuwapatia wananchi wetu huduma ya Habari na Mawasiliano.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema ujenzi wa kituo hicho umegharimu shilingi milioni 430 kwa udhamini wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Amesema maeneo mengine ambayo miradi inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa TBC na UCSAF ni  katika wilaya za Ngara (Kagera), Kyela (Mbeya), Ruangwa (Lindi), Kilombero/Mlimba (Morogoro), Ludewa (Njombe), Mlele (Katavi),  Makete (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mbinga (Ruvuma) na Ngorongoro (Arusha).

Naye, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashimba amesema serikali kupitia mfuko huo utaelendelea kuboresha mawasiliano na usikivu wa huduma za radio kwa kuwafikia wananchi kote nchini.

AwaliMkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayoub Ryoba amesema, shirika hilo limejipanga kuhakikisha wanaendelea kuuhabarisha umma wa wa Tanzania kwa uhakika na weledi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya shirika hilo.



 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango