Serikali, NMB zasaini makubaliano kukuza kilimo

DODOMA

WIZARA ya Kilimo na Benki ya NMB, zimeingia makubaliano ya kukuza sekta ya kilimo nchini ambapo benki hiyo imetenga shilingi bilioni 120 kwa ajili ya mikopo ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao vijijini na kukuza kilimo nchini.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makuliano hayo iliyofanyika katika hoteli ya Morena mjini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliipongeza benki ya NMB kwa juhudi za kusaidia ukuzaji wa sekta ya kilimo nchini.


Alisema moja ya changamoto wanayokabiliana nayo wakulima nchini ni mazao yao kupoteza ubora kabla ya kufika sokoni kutokana na mazingira mabaya ya kuhifadhi hivyo makubaliano hayo yanakwenda kupunguza changamoto hiyo.

“Kule vijijini ukiona magunia mengi ya mazao yamewekwa kwenye eneo la mashine za kusaga, usifikiri kuwa ni mali ya mwenye mashine hiyo. Magunia hayo ni mali ya wakulima yamehifadhiwa hapo baada ya kukosa ghala la kuhifadhia na yanapofika sokoni, yanakuwa yamepoteza ubora na thamani yake,” alisema Bashe.

Aidha Waziri Bashe alisema wizara yake inatambua matatizo na changamoto zinazowakabili wakulima na imejipanga kukabiliana nayo kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kama benki ya NMB.

Alisema maghala yatakayojengwa kupitia vyama vya ushirika, Wizara ya Kilimo itasimamia kuhakikisha dhamira ya serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kukuza sekta ya kilimo, inatimia.

Alisema maghala hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 100, 200 hadi 300 ili wakulima waweze kutunza mazao yao na yabaki kwenye ubora kabla ya kufika sokoni.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, (wa kwanza kutoka kulia) alisema wamefikia makubaliano hayo baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya pande mbili hizo.


Alisema mkopo huo ni mwendelezo wa juhudi za benki hiyo kuuza sekta ya kilimo nchini ambapo mwezi Oktoba mwaka jana, benki hiyo ilitenga shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kukopeshwa wadau wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa riba isiyozidi asilimia 10.

“Mpaka sasa zaidi ya shilingi Bilioni 80 zimeshatolewa kwenye mikopo hii. Baada ya kuona shilingi bilioni 100 zinaisha, tumeona tuongeze nyingine kama hizo ili kuongeza utoaji wa mikopo kwa wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiliamali katika sekta hizi,” alieleza Zaipuna.

Wakati akizindua mpango wa uimarishaji wa sekta ya kilimo iliyoenda sambamba na ugawaji wa pikipiki kwa maofisa ugani na vitendea kazi mbali mbali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitoa wito kwa taasisi za kifedha kusaidia ukuzaji wa uwekezaji kwenye kilimo kuongeza tija.

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango