Ujerumani kusaidia utafiti wa maji Z'bar
ZANZIBAR
SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali
ya Shirikisho la Ujerumani zimetiliana saini mkataba wa ruzuku ya utafiti na
upembuzi yakinifu katika sekta ya maji unaolenga kujua ubora na wingi wa maji
yanayopatikana Zanzibar.
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Johannes Sperrfechter ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi na ushirikiano wao ambao unalenga kujenga maisha bora ya Wazanzibari.
Alisema
hatua hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano mpya wa kimaendeleo kati ya Ujerumani
na Zanzibar uliozinduliwa mwezi Januari 2022 kwa pamoja na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Balozi wa
Ujerumani.
Katika
uzinduzi huo, ujerumani iliahidi kuisaidia Zanzibar katika maeneo mbali mbali
yakiwemo ya uimarishaji wa sekta zinazohusiana na maisha ya watu.
Balozi
Johannes alisema mchakato wa utafiti na upembuzi yakinifu umeshaanza na
masharti ya mkataba yanakaribia kukamilika ambapo mamlaka ya Maji Zanzibar
(ZAWA) na wadau wengine wa maendeleo watahakikisha wanaongeza ufanisi.
“Matarajio
yetu kupitia mpango huu ni kupata maarifa muhimu ya usimamizi endelevu wa
rasilimali za maji Zanzibar kwa kufanya utafiti wa maji yaliyopo chini ya ardhi,”
amesema balozi Johannes.
Kwa
upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada
Mkuya Salum alisema Zanzibar pamoja na kuwa ni nchi ya visiwa lakini imekuwa
ikibabiliwa na changamoto ya maji kwa wananchi wake.
Alisema
kutokana na hali hiyo ndipo Serikali ya Ujerumani imekubali kuwapatia msaada wa
Euro milioni 6.6 sawa na shilingi Bilioni 1.7 za Tanzania zitakazotumika kwa
utafiti huo pamoja na mambo mengine yanayolenga kujua ukubwa wa tatizo hilo
nchini.
Aliipongeza
serikali ya Ujerumani kwa kuamua kusaidia mradi huo ambao Zanzibar inakwenda
kutekeleza kwa vitendo mpango wa maendeleo wa miaka mitatu na mpango mkuu wa
2025 unaolenga kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama Zanzibar.
“Kwa
upande wetu Serikali tutausimamia utekelezaji wa mradi huu utakaotekelezwa maeneo
mbali mbali ya na kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.
Hafla ya utiaji wa saini ilifanyika katika ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Kinazini Zanzibar na kushuhudiwa na viongozi hao wa serikali ya Zanzibar na Ubalozi wa Ujerumani nchini.
Comments
Post a Comment