Wizara yahimizwa kukamilisha ujenzi ofisi za ZBS

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya bajeti ya Baraza la Wawakilishi imeitaka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa ofisi za Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) ili kuipa uwezo wa kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

MWENYEKITI wa Kamati ya bajeti, Abdalla Hussein Kombo (kulia) akiongoza kikao cha kamati na viongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa ZBS Yussuph Majid Nassor, katikati ni Katibu Mkuu  Dk. Islam Seif.

Akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo, uongozi wa wizara na taasisi hiyo, kilichofanyika katika ofisi za ZBS Amani, Mwenyekiti wa kamati hiyo Abdalla Husein Kombo, alieleza kuwa iwapo taasisi hiyo itaongezewa uwezo, mapato na ufanisi utaongezeka.

Alieleza kuwa ujenzi wa ofisi za taasisi hiyo unaojumuisha maabara za kupimia na kuchunguza ubora wa bidhaa mbali mbali ni sehemu muhimu ya mafanikio ya taasisi hiyo hivyo ni vyema ikazingatia umuhimu wa kuukamilisha kama ilivyopanga.

“Mtakapokua na maeneo mazuri ya kufanyia kazi na maabara za kutosha naamini mtaongeza ufanisi lakini kuongeza mapato ambayo sasa wanalipwa mawakala wanaowafanyia kazi ambayo wenyewe mnaweza kuifanya,” alieleza kombo.

Aidha alipongeza uwekezaji uliofanywa na kuitaka taasisi hiyo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wajumbe wa kamati hiyo na kufanya kazi kwa lengo la kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Kuhusu kutambulika kwa cheti cha ithiubati ubora kinachotolewa na ZBS, Kombo alisema kuna umuhimu wa ZBS kufanya juhudi za makusudi kuhakikisha ubora wa hali ya juu wa bidhaa ili kutambulika nje ya nchi.

Akiwasilisha taarifa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi ya viwango Zanzibar kwa kipindi cha Julai – Machi 2021/2022, mkurugenzi wa zbs, mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Yusuph Majid Nassor, alieleza kuwa katika kipindi hicho viwango 90 vya bidhaa na huduma mbali mbali viliandaliwa.

Alivitaja baadhi ya viwango hivyo ni viwango 40 vya bidhaa za vyakula, viwango 25 vya bidhaa za kemikali, viwango 22 vya bidhaa za uhandisi mitambo na vyombo vya moto, viwango 10 vya mazingira, viwango vine vya huduma na viwango vitano vya bidhaa za umeme na elektroniki.

Aidha Yussuph alieleza kuwa pamoja na mafanikio, katika kipindi hicho taasisi imekabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya kukosekana kwa mifumo ya ndani ya TEHAMA na kutokuwepo kwa muongozo wa utoaji mizigo katika bandari.

WAJUMBE wa kamati ya bajeti wakifutia na kuchambua taarifa iliyowasilishwa.

Akizungumzia mradi wa uimarishaji wa ofisi na maabara maruhubi, Yussuph alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 5.2 pamoja na VAT ambapo hadi sasa jumla ya shilingi 2,765,048,528.86 zimeshalipwa.

“Mradi huu utakapomalizika utaondoa chqangamoto ya uhaba wa ofisi kwani utaanzisha maabara mbali mbali ikiwemo ya vifaa vya ujenzi kama vile lami, saruji, mabomba ya maji safi, udongo, kokoto na nyenginezo,” alieleza mkurugenzi huyo.

Akizungumza katika kikao hicho, katibu mkuu wa wizara hiyo, dk. Islam seif salim, aliahidi kuyafanyia kazi mapendekezo na maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo.

Alieleza kuwa katika mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022, wizara hiyo imepanga kukamilisha ujenzi wa ofisi za taasisi hiyo pamoja na kuanza ujenzi wa eneo la maonesho ya biashara Dimani/Nyamanzi.

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango