TAARIFA MAALUM KWA WAANDISHI WA HABARI
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAOMBI YA WAANDISHI KWA RAIS WA
ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI DK. HUSSEIN ALI MWINYI
Awali ya yote
napenda kutumia fursa hii kwa niaba ya Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa
Habari Zanzibar (ZPC), kuwajullisha ya kwamba baadhi ya mambo yaliyowasilishwa na
waandishi wa habari mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kikao cha tarehe 18/05/2022 yameanza
kufanyiwa kazi.
Katika kikao hicho
cha faragha kilichofanyika katika Ikulu ya Zanzibar, waandishi wa habari walipata
fursa ya kuzungumza na Rais mambo mbali mbali yanayohusu mwendendo na hali
halisi inayohusiana na tasnia ya habari nchini, hali tunayoamini imeongeza
uelewa wa kiongozi huyo wa nchi na wasaidizi wake juu ya mazingira ambayo
waandishi wa habari wa Zanzibar wanayofanyia kazi.
Pamoja na maelezo
ya waandishi ambayo baadhi yao yalipatiwa majibu na kutolewa ufafanuzi wakati
wa kikao hicho, pia waandishi waliwasilisha ombi mahususi kuhusu nafasi za
mafunzo ili kujiongezea ujuzi na utaalamu kuimarisha ufanisi wa kazi zao.
Kuhusiana na ombi
hilo, napenda kuwajulisha kwamba jambo hilo limeanza kufanyiwa kazi na kutolewa
maelekezo kupitia barua iliyowasilishwa kwa ndugu Abdallah A. Mfaume, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari
Zanzibar (ZPC) tarehe 20/08/2022 na kutolewa maelekezo kwamba tunapaswa
kutumia fursa za masomo zilizotangazwa na ubalozi mdogo wa India nchini.
Katika barua hiyo
iliyoambatanishwa na maelekezo kutoka ubalozi wa India nchini, inawataka
waandishi wa habari kutumia fursa zinazotolewa na taasisi ya ITEC kupitia
mpango wa ushirikiano baina ya Tanzania na India kwa mwaka 2022/2023 (Aprili 2022 – Machi 2023).
Hivyo waandishi
wenye hamu ya kupata mafunzo hayo wanatakiwa kufanya maombi ya masomo
wanayotaka kwa kutembelea tovuti ya taasisi hiyo ambayo ni https://www.itecgoi.in
ili kupata mpangilio wa masomo na mafunzo yanayotolewa kupitia mpango huo.
Baada ya
kukamilisha maombi, muombaji atalazimika kupakua (download) fomu ya maombi na
kuiwasilisha katika Wizara ya nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala wa Umma
na Utawala bora au Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
ofisi ya Zanzibar na tunashauri nakala ya maombi hayo yawasilishwe ZPC kwa
ajili ya kumbukumbu.
Kwa taarifa hii,
ninawashajihisha waandishi wote wenye utashi, hamu na sifa ikiwemo ya umri wa kati ya miaka 25 – 45 kutumia
fursa hii kikamilifu lakini wenye zaidi ya umri huo kupitia tovuti hiyo na
kuangalia kozi za mafunzo yanayotolewa na taasisi hiyo.
Aidha kwa niaba ya
waandishi wa habari wa Zanzibar, tunashukuru hatua hizi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuiimarisha sekta ya
habari na tunamuomba aendelee kutoa kipaumbele kwa sekta hii kama kichocheo cha
maendeleo ya nchi na watu wake.
Ni matumaini yangu
kwamba, hatua hizi zilizochukuliwa katika kipindi kifupi, kitachochea kasi ya
waandishi kujituma na kujitokeza kuomba mafunzo yanayotolewa na taasisi hiyo
hata yale yaliyopo nje ya kada ya uandishi wa Habari.
Kwa mara nyengine
natoa shukrani na pongezi kwa waandishi wa habari waliohudhuria kikao na mhe.
Rais kwa kuonesha haja ya kuijiendeleza na kuiendeleza kada ya uandishi wa habari,
jambo ambalo limekuwa likisisitizwa na vyama vyetu vya kitaaluma, hivyo naomba,
tusipoteze fursa iliyotolewa.
Ahsanteni.
Imetolewa na:
Mwinyimvua A. Nzukwi,
Katibu Mkuu – ZPC.
Comments
Post a Comment