Waandishi watakiwa kuwa makini matumizi mitandao
WAANDISHI
wa habari wametakiwa kutanua wigo katika matumizi ya mitandao ya kijamii ili
kurahisisha utendaji wao wa kazi na kuleta tija.
MWENYEKITI wa klabu ya waandishi wa
Habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Abdulrahman Mfaume, alisema hayo alipokuwa
akifungua kongamano la wadau wa habari ikiwa ni miongoni mwa shudhuli za maadhimisho
ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ngazi ya klabu.
Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia
kwa kiasi kikubwa kubadilisha jamii kutumia mitandao hiyo kwa faida badala ya hasara
kutokana na jukumu kubwa la kuelimisha jamii na kuleta mabadiliko katika nchi.
Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo
aliiomba serikali kuendelea kushirikiana na wadau wa habari kufanya mapitio ya
sheria, sera na kanuni zinazosimamia sekta ya habari ili kuondosha changamoto
zinazokwaza uhuru wa Habari na Uhuru wa kujieleza.
Hata hivyo aliwasisitiza waandishi
wa habari kuzalisha habari na vipindi bora ili vyombo vya habari viendelee kuwa
daraja la kupashana Habari na kupeana mrejesho kati ya serikali na wananchi.
Akizungumzia mafanikio maadhimisho ya
siku hiyo kitaifa na kimataifa, Mfaume alisema yamesaidia kwa kiasi kikubwa
kupunguza baadhi ya vikwazo na changamoto zilizokuwa zikiwakabili waandishi na
vyombo vya habari.
Akitaja miongoni mwa mafanikio hayo
kuwa ni pamoja na mauaji ya waandishi wa habari na watendaji wa vyombo vya
habari, kuteswa kinyama, kunyimwa habari, maslahi duni, ukatili na
udhalilishaji wa wanahabari hasa wanawake.
Mbali na hayo alisema juhudi zaidi
zinahitajika ili kuona vikwazo vyote visivyo vya msingi vinaondolewa ili kuona
habari iendelee kuwa bidhaa muhimu kwa umma.
Mapema Katibu wa ZPC, Mwinyimvua
Abdi Nzukwi, alisema kupitia siku hiyo, klabu hiyo imekuwa ikifanya kongamano
na mikutano mbali mbali kwa waandishi wa habari ili kujadili mafanikio, changamoto
na vikwazo vinavyowakwaza waandishi ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi hatua kwa
hatua.
Wakiwasilisha mada katika kongamano
hilo lilihudhuriwa na maofisa habari, waandishi wa habari na wadau wa Habari,
muhariri wa shirikia na magazeti ya serikali, Juma Khamis Juma na Katibu wa
kamati ya muda ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ofisi ya Zanzibar, Salma Amir
Lusangi, waliwataka waandishi kusimamia misingi ya kazi zao ili kujiepusha
kuingia katika matatizo.
“Pamoja na kwamba baadhi ya sheria
zina mapungufu, ipo haja ya kuchukua juhudi ya kuzisoma ili kujiepusha kuingia
kwenye mtego wa kuzivunja,” alieleza Khamis.
Wakichangia mada zilizowasilishwa
kwenye kongamano hilo, baadhi ya waandishi hao walipokuwa walisema licha ya
kuadhimishwa kwa siku hiyo kila mwaka lakini bado waandishi wa habari wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokua na mikataba ya ajira na
stahiki zao za msingi.
Aidha waliiomba ZPC kushirikiana na taasisi nyengine za habari kuendelea kusimamia misingi ya taaluma pamoja na kuanzisha utaratibu wa kukutana na kutathmini hali ya uandishi wa habari kama njia mojawapo ya kuimarisha upatikanaji wa uhuru wa habari.
Kongamano hilo la siku moja liliandaliwa
na ZPC kwa ufadhili wa Shirika la kimataifa la Misaada la Sweden (SIDA)
kupitia mpango wa kuimarisha klabu za waandishi wa habari unaotekelezwa na
Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Comments
Post a Comment