'Andikeni habari zitakazochochea maendeleo '
NA MWANDISHI WETU
WANAHABARI nchini wametakiwa kubadilika na kuandika habari zitakazochochea maendeleo ya nchi na watu wake.
Wito huo Umetolewa
na Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Hassan Khatib Hassan, (wa katitaki pichani) alipokua akifungua mafunzo ya waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari yaliyoandaliwa
na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) kwa kushirikiana na shirika la
Internews Tanzania, yaliyofanyika katika ukumbi wa Uhuru, Kariakoo Zanzibar.
Alieleza kuwa
vyombo vya habari ni muhimu kwani vinaweza kuandika habari zenye kuibua hamasa
ya wananchi kufikia dhamira ya serikali na kufichua maovu dhidi ya maendeleo ya
nchi na watu wake.
Hassan aliongeza
kuwa wananchi walio wengi wanasikiliza na kufuatilia vyombo vya habari
wakiamini kuwa watapata taarifa za ukweli na zinazozingatia weledi na sio
taarifa za kubuni ama kughushi.
“Iwapo mtajikita zaidi kutaka kuwafurahisha
wasomaji na wasikilizaji au watazamaji basi tunaweza kufika pahala tukapoteza
malengo ya kazi yetu tunayoifanya,” alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha aliwataka
waandishi wa habari kuacha tabia ya kusubiri habari za kuitwa na wanasiasa au
viongozi wa taasisi badala yake waanzishe utaratibu wa kujitafutia habari, jambo
linaloongeza thamani na uhalisia wa tasnia hiyo.
Alisema imefika
wakati kuhakikisha waandishi wanaandika habari za uchunguzi na kuripoti taarifa
kuhusiana na masuala ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na udhalilishaji kwa
kuyakemea kwa kuwa ndio yanayorejesha nyuma maendeleo ya nchi yao.
“Ingelipendeza na
kutupa heshima kubwa ndani ya tasnia yetu iwapo sisi waandishi tungekuwa wa
mwanzo kubaini mambo au kuwa sababu ya serikaili kutoa ufafanuzi ndani ya
serikali kwa kuwa na utaalamu wa kudadisi kuchunguza na hatimae kuibuka na
mambo yenye uhakika,” alisema Hassan.
Akimkaribisha Mkurugenzi huyo, Mwenyekiti wa ZPC, Abdallah Abdulrahman Mfaume, aliwasisitiza wanahabari wanapoandika habari zenye takwimu data kuhakikisha zinakua sahihi ili kuleta matokeo chanya na kupata usalama wa nchi badala ya kuwa ndio chanzo cha kuleta taharuki.
Aidha, aliwahimiza
kuendelea kuweka mizania kwenye Habari zao kwa kuhusisha pande zote ili kuepusha
matatizo yasiyokuwa na tija.
Aidha aliwaomba
washiriki wa mafunzo hayo, kuacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea badala yake wajitolee
kwa moyo wa dhati ili kuleta mabadiliko kwa jamii inayowasikiliza na taifa kwa
ujumla.
Mafunzo hayo
yaliyoshirikisha waandishi wa Habari 30, mada za uandishi wa habari za
uchunguzi, usahihi wa takwimu (data), habari za jinsia na namna ya kufungua
mashauri ya kimkakati kulinda Uhuru wa Habari ziliwasilishwa na Wakufunzi wa
vyombo vya habari, Imane Duwe, Ali Mwadini na Juma Khamis.
Comments
Post a Comment