NMB yakabidhi gawio la 30.7b/- serikalini
NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, ameyataka mashirika ambayo serikali ina hisa kuhakikisha yanatoa gawio la serikali pamoja na taasisi zinazotakiwa kutoa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mujibu wa sheria zifanye hivyo kwa wakati.
Makamu wa
Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya kupokea gawio la shilingi bilioni 30.7
kutoka kwa benki ya NMB iliyofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma Juni
15 2022.
Alisema mashirika
yanayotegemea ruzuku kutoka mfuko mkuu wa serikali yanapaswa kuwa na mikakati madhubuti inayotekelezeka ili kupunguza
utegemezi kwa serikali na kumuagiza Msajili
wa Hazina kuhakikisha wakuu wa taasisi hizo
wanatekeleza maagizo hayo.
Dk. Mpango
alieleza kuwa, serikali itaendelea kuweka mazingira endelevu ya biashara kwa
sekta ya fedha nchini na kuipongeza benki ya NMB kwa kuendelea kuchangia
maendeleo ya jamii sambamba na kusaidia ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa
kuimarisha mifumo ya ukusanyaji.
Aidha aliwashauri
watendaji wa benki hiyo kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuongeza fursa
za ajira kwa vijana na wanawake na kuimarisha huduma za kijamii kwenye sekta mbali mbali
kama afya, elimu na utunzaji wa mazingira na
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na tabia watu.
Nae Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Wizara itaendelea kusimamia
maelekezo na kuhakikisha taasisi za serikali ambazo serikali ina hisa zinatoa gawio.
“Serikali itaendelea
kushirikiana na taasisi zote za sekta binafsi ili kuhakikisha zinafanya kazi
vizuri na kuwasilisha gawio la serikali,” alieleza Dk. Nchemba.
Awali akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais, Afisa Mtendaji Mkuu wa
NMB, Ruth Zaipuna, alisema faida ya benki hiyo baada ya kodi katika kipindi cha
2021 iliongezeka kwa asilimia 41 na kufikia shilingi bilioni 290.
Alieleza
kuwa, kiasi hicho ni kikubwa ikilinganishwa na shilingi bilioni 206 za mwaka
2020 ambapo idadi ya akaunti za wateja iliongezeka hadi kufikia shilingi milioni
5 ikilinganishwa na milioni 4 za mwaka 2020.
“Katika kuhakikisha benki
inaendelea kuwa na maendeleo endelevu, tumeongeza mtaji wa benki hadi kufikia shilingi
trilioni 1.3 na benki iliendelea kuwa na ufanisi na kuweka rekodi ya uwiano wa
gharama za uendeshaji na mapato, kufikia asilimia 46,” alisema Zaipuna.
Zaipuna alisema kwa
mwaka 2021, benki ilipata tunzo saba za kimataifa, ikiwemo ya benki bora nchini
kwa miaka tisa mfululizo iliyotolewa na jarida la kimataifa la ‘Euromoney’.
“Aidha
hadi mwishoni mwa mwaka 2021, mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 4.3 imetolewa
kwa wakulima, wafanyabiashara wadogowadogo na wa kati na watu binafsi,”
aliongeza Zaipuna.
Alisema mafanikio
hayo yalitokana na kuimarika kwa uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, huduma
za wakala, zilizoongezeka na kufikia mawakala 10,194 ukilinganishwa na mawakala
8,410 waliokuwepo 2020.
Nae Mwenyekiti wa
bodi ya wadhamini ya NMB, Dk. Edwin Mhede alisema ongezeko la faida kwa benki
hiyo linatokana na uimara na umadhubuti wa uongozi na kwamba wanajivunia kuwa
na Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna.
Akitaja mafanikio ya
kipindi cha miaka mitano, mhede alieleza kuwa yamekuwa yakipanda kila mwaka
ambapo kwa mwaka 2020 benki ilitoa gawio la shilingi 20.8 bilioni, huku mwaka 2019
shilingi bilioni 15.6 zilitolewa.
“Tunatarajia kwa
mwaka wa 2022 kuwa na gawio nono zaidi kwani katika kipindi cha miezi mitatu ya
mwanzo, benki imepata faida kubwa inayolingana na faida ya mwaka mzima katika
kipindi cha miaka ya nyuma,” alieleza Mhede.
Comments
Post a Comment