Wanufaika TASAF wataja mafanikio
NWANDISHI WETU, PEMBA
WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), kisiwani Pemba wamesema miradi waliyoibua imewakomboa kiuchumi na kumudu gharama za kusomesha watoto wao skuli.
Walisema miradi mingi waliyoianzisha kutokana na ruzuku wanazopokea kupitia mpango huo, imewatoa kutoka katika dimbwi la umasikini na sasa wana uhakika wa kupata kipato cha kujikimu kimaisha.
Mmoja ya wanufaika hao, Bahati
Vuai Haji wa kijiji cha Kwareni Vitongoji, mkoa wa Kaskazini Pemba alieazisha
biashara ya mgahawa wa chakula, alisema kuwa kabla ya kuwezeshwa na TASAF hali
yake kiuchumi ilikuwa ngumu.
Alisema baada ya kupitia ruzuku hiyo
aliweka akiba na kuanzisha biashara ya bagia na kujiunga katika vikundi vya
kuweka na kukopa hatimaye kuazisha mgahawa wa chakula (Mamantilie) ambapo kwa
sasa ndio kazi inayoendesha familia yake ya watoto watano.
“Nashukuru hivi sasa napata
fedha familia yangu inapata huduma ya chakula na nyengine maana kabla ya
kupatiwa ruzuku nilikuwa Napata shida kuwahudumia watoto wangu kwa sababu baba
yao hana msaada wowote,” alisema.
Bahati alisema biashara hiyo imemuwezesha kununua kiwanja,
kusomesha watoto wake na kulisha familia angalau kwa milo miwili kuliko
ilivyokua kabla.
Hata hivyo mnufaika huyo alisema
kuwa bado mtaji wake ni mdogo hivyo anahitaji fedha kwa ajili ya kuboresha
biashara zake ili huduma anayoitoa kuwa na ubora.
Mnufaika mwengine Saumu Amour
Muhammed, mkaazi wa kijiji hicho, alisema baada ya kupata ruzuku ya shilingi 84,0000
kutoka TASAF alianza kufanya biashara ndogo ndogo na kujiunga na vikundi vya
kuweka na kukopa na faida aliyoipata akaanza na kilimo cha mboga na matunda.
Alisema kilimo hicho kimekuwa ni
tegemezi kwa familia yake lakini changamoto kubwa aliyonayo ni uhaba wa maji
kwa ajili ya umwagiliaji wa kilimo chake na kuiomba Serikali kuendelea
kuwapatia elimu na mitihaji ili kukuza biashara zao na kutoa ajira kwa watu
wengine.
Comments
Post a Comment