Dk. Mwinyi kuongoza wadau sekta ya maji kujadili changamoto, mafanikio

NA MWANDISHI WETU

WADAU wa sekta ya maji wa ndani na nje ya Zanzibar wanatarajiwa kukutana Septemba 14 na 15, mwaka huu katika Kongamano la   Kimataifa la Maji Zanzibar.

Kongamano hilo linalotarajiwa kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, litafanyika katika hoteli ya Goldern Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake Maisara, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaibu Hassan Kaduara, alisema wadau wa sekta ya maji wapatao 2,000 kutoa ndani na nje ya nchi wakiwemo, watafiti, watunga sera na watendaji wa wizara na idara za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na Zanzibar watashiriki.

Alieleza kongamano hilo ni sehemu ya kuunganisha Juhudi za Utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Uwekezaji katika sekta ya maji Zanzibar (ZanWIP) wa miaka mitano unaoanza 2022 hadi 2027 uliozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Alisema, hatua hiyo ni utambuzi wa mawazo, dhana na ubunifu ili kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji katika visiwa vya Zanzibar.

Aidha alisema serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Mwinyi, kupitia wizara yao, inaendelea na mipango na mikakati ya kuendeleza na kimageuzi katika sekta ya maji ili kwenda sambamba na ahadi ya ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.

“Kupitia kampeni zake wakati akinadi sera zake, Rais dk. Mwinyi aliahidi wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba kuwa wataondokana na shida ya maji, hivyo kongamano hili ni moja kati ya njia za kuainisha changamoto za ujumla katika sekta ya maji,” alieleza Waziri huyo.

Sambamba na hayo, Kaduara alisema kupitia kongamano hilo, watafiti watawasilisha mapendekezo ya tafiti zao na kujadiliana juu ya mbinu za kisayansi na kiutafiti zitakazotoa muelekeo na kuibua dhana mpya ya miradi pamoja na ubunifu utakaosaidia usimamizi endelevu wa sekta ya maji.

Kongamano hilo limeandaliwa na Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kushirikiana na taasisi ya Global Water Partnership Tanzania na wadau mbali mbali likiwa na kauli mbiu ‘Usimamizi endelevu wa rasilimani mji chini ya ardhi katika mabadiliko ya tabianchi’.

 

 


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango