Euro 10.1M kuimarisha usalama wa chakula Tanzania
Na Saida Issa,DODOMA
SERIKALI imezindua mradi wa miaka mitatu na miezi sita wa uboreshaji huduma za afya ya mimea Tanzania utakaogharibu kiasi cha EURO milioni 10.1 ikiwa ni hatua za kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Hayo
yalibainishwa Jijini Dodoma na Naibu waziri wa Kilimo Antony
Mavunde,wakati akizungumza katika uzinduzi huo.
Alisema Februari 16, 2021, serikali ya kupitia Wizara ya Fedha na Mipango
iliingia mkataba wa kutekeleza mradi wa Kuimarisha Afya ya Mimea na Jumuiya ya
Umoja wa Ulaya (EU).
Mradi
huu wa miaka mitatu na miezi sita unafadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya
(EU) kupitia Mfuko wake wa Maendeleoa (EDF), Shirika la Umoja w a Mataifa la
Kilimo na Chakula (FAO) na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Aidha,
FAO ni wasimamizi wa mradi na utekelezaji hufanywa na serikali ya Tanzania
kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viutilifu (TPHPA) iliyo chini ya Wizara ya
Kilimo”alisema Mavunde.
Alisema
kuwa mradi huo unatekelezwa kwa bajeti ya jumla EURO Milioni 10.1 ikiwa ni
mashirikiano ya ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EUR Milioni 9.5),
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula – FAO (EUR 350,000) na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (EUR 250,000).
Mavunde,
alisema mradi huo unalenga kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa kuimarisha
mfumo wa ukaguzi na utoaji wa vyeti vya usafi wa mazao yanayosafirishwa kwenda
nje ya nchi.
Pia, mradi
huo unalenga kudhibiti visumbufu vigeni kwa kuhakikisha mazao yanayoingia au
kutoka nchini yana ubora unaokidhi viwango vya masoko ya kimataifa.
“Nachukua
fursa hii kuwashukuru Umoja wa Jumuiya ya Ulaya (EU) na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) kwa kufadhili na kusimamia fedha za mradi
huu muhimu. Ni imani yetu kuwa malengo yaliyopangwa yatafikiwa na hivyo
kuongeza upatikanaji wa masoko ya kimataifa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa
Taifa na wa mtu mmoja mmoja,”alisisitiza Mavunde.
Vile
vile, alisema mradi huo ulitokana na ukaguzi uliofanyika hapa nchini mwaka
2017, katika mifumo maalum ya udhibiti wa mimea na mazao yanayosafirishwa
kwenda nchi za Umoja wa Jumuiya ya Ulaya.
“Ukaguzi
huo ulibaini mapungufu yalikuwa sehemu ya Afya ya Mimea katika maeneo
yafuatayo, maarifa madogo kwa wakaguzi wa afya ya mimea kuhusu matakwa ya usafi
wa mazao na bidhaa za kilimo zinazoingizwa katika nchi za Umoja wa
Ulaya,kukosekana kwa mfumo wa kufanya kukusanya takwimu za visumbufu vya mazao,kukosekana
kwa maabara maalum zenye uwezo wa kufanya uchunguzi muhimu ili kuthibitisha
cheti cha usafi wa mimea kinachotolewa kwa mimea na mazao yanayokidhi vigezo na
masharti ili kufikia masoko ya kimataifa,"alisema.
“Kutokuwepo
kwa utaratibu wa kutambua masuala ya usafi wa mimea na maarifa madogo kuhusu
matakwa yaliyopo ya ubora wa mimea na mazao wakati wa usafirishaji kufikia soko
husika”alieleza.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya mimea na Viwatilifu
Tanzania (TPHPA), Dk. Efraim Njau, alisema sekta ya kilimo ni muhimu sana
ambapo imeajiri zaidi ya asilimia 67 ya watanzania na kuchangia takribani
asilimia 29 ya pato la taifa.
“Matokeo
tarajiwa ya mradi huu ni kuziongezea uwezo maabara za mamlaka kujenga,
kukarabati na kuweka vifaa katika maabara za Mamlaka, kuimarisha mfumo wa
ufuatiliaji wa visumbufu na masalia ya viuatilifu katika mnyroro wa thamani ya
uzalishaji wa mazao hususan ni yale mbogamboga na matunda,” alisema.
Mwakilishi wa FAO, Nyebenyi Tipo, alisema mradi huo umelenga kuhakikisha usalama wa chakula hasa kwa mazao yanayovuka mipaka kwa kuhakikisha yanakuwa na ubora.
Comments
Post a Comment