JMKF, PIT zawanoa wasichana kufikia ndoto zao

DAR ES SALAM

WASICHANA 40 kutoka skuli na vyuo mbali mbali wapepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwawezesha kujikomboa kimaisha.


Mafunzo hayo yaliyopewa jina la ‘Wasichana Washika Hatamu’ yaliandaliwa na taasisi za Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) kwa kushirikiana na shirika la Plan International Tanzania (PIT), yalifanyika kwa siku mbili katika hoteli ya Regency Park jijini Dar es salaam.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa JMKF, Vanessa Anyoti, alieleza kwamba imekuwa jukwaa muhimu katika kutambua haki za msichana na changamoto kubwa anazopambana nazo duniani.



 Alieleza kwamba kwa sasa kuna wito wa kuchukuliwa kwa hatua za makusudi, kuleta mageuzi  ya kijamii na kisiasa ili kuondoa vizuizi vya ubaguzi na chuki vinavyoendelea kurudisha nyuma maendeleo ya wasichana.

 

“Tanzania inaungana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kukuza ufahamu wa jamii juu ya masuala yanayowakabili wasichana na kuwapatia fursa ya kupaza sauti zao,” alisema mkurugenzi huyo.





Aliongeza kuwa duniani kote wasichana wanaendelea kukabiliana na changamoto za uongozi, elimu, masuala ya afya ya akili na ukatili wa kijinsia hivyo kuna haja ya kuwajengea uwezo ili wawe mawakala wakuu wa mabadiliko katika jamii zao.

 

Mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya shughuli za kuelekea kilele cha siku ya kimataifa ya mtoto wa kike inayoadhimishwa kila ifikapo Oktoba 11 ya kila mwaka yanalenga kuwawezesha wasichana na kukuza sauti zao. 


 

Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na wadau wengine, taasisi yake itaongeza uwezo wa vijana wasichana wa  kujiamini,  kutambua afya ya akili, kukuza ustawi wao hususani katika masuala ya lishe na ukakamavu.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni ya kutambua haki za mtoto wa kike pamoja na ufahamu wa sheria za nchi juu ya maswala yanayowahusu chini ya kauli mbiu ya maadhimisho hayo Duniani inayosema; ‘Wakati wetu ni sasa — haki zetu, mustakabali wetu’.


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango