Mbunge ataka vijana kutambua nafasi zao kwenye maendeleo
NA SAIDA ISSA, DODOMA
MBUNGE wa Viti Maalum, Nusrat Hanje, amesema katika kuhakikisha mchango wa vijana unaonekana kwenye maendeleo ya taifa vijana wanatakiwa kutambua nafasi yao na nguvu ya ushawishi waliyonayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi
wa ‘Vijana Makini’, jijini Dodoma alisema serikali ina wajibu wa kutengeneza
mbinu wezeshi kwa kuwafanya vijana wanajibika kwa kua kundi hilo lina idadi
kubwa ya watu nchini.
"Vijana ni sehemu kubwa katika nchi
yetu, nikiwa Mbunge kijana naishauri serikali yetu kuwatengenezea mbinu wezeshi
vijana hawa ambao ndio taifa la kesho,” alieleza Mbunge huyo.
Aliongeza kuwa iwapo serikali itaweka
misingi imara na thabiti kwa vijana wa leo hapo baadae hakutakuwa na changamoto
katika taifa kwani watakua imewekeza katika eneo salama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi,
Uratibu na Uwezeshaji kiuchumi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye ulemavu, Eliakim Mtawa alisema mara nyingi vijana ndio wenye tatizo
kwani wanapopata fedha huzitumia kwa malengo yasiyokusudiwa.
“Serikali inatoa hela kwenu lakini nyinyi
ni shida pia hamshiriki katika vikao vya chini kujadili mambo yenu bali mnakuja
kwenye ngazi za juu na kudai wakati kule chini hampo nani atayasemea mambo
yenu,” alihoji Mtawa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Dira
ya Vijana Tanzania (TYVA), Yusuph Bwango, alisema lengo la mradi huo ni kuhakikisha
vijana wanakuwa na ushiriki madhubuti katika ushwawishi na utetezi wa masuala yanayowahusu na kwenye mchakato wa
bajeti ya serikali.
Alisema mradi huo unalenga kujumuisha taasisi
za vijana mbali mbali za vijana zitakazounda mwamvuli utakao wawakilisha kwenye
jukwaa la utetezi wa bajeti ya vijana.
Comments
Post a Comment