NMB, Bunge SC hapatoshi 'Kivumbi na Jasho' season II

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

MSIMU wa pili wa Bonanza la ‘NMB Kivumbi na Jasho,’linalokutanisha timu za michezo za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya NMB, linafanyika Jumamosi Septemba 17, 2022 jijini Dodoma.

Bonanza hilo linafanyika baada ya Septemba 16, mwaka huu benki hiyo kukabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa timu ya Bunge SC.

Akizungumza wakati akipokea msaada wa vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Bunge SC, Tarimba Abbas, alieleza kuwa bonanza hilo linalenga kujenga na kuimarisha mahusiano mema baina ya bunge na NMB.

Aidha Tarimba aliahidi kulitumia bonanza hilo kama kama ilivyofanya msimu uliopita kuzipa makali timu za bunge zinazojiandaa na mashimdano ya mabunge ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA 2022).

"Tunatambua na kuthamini malengo ya bonanza hili, lakini tuwe wazi kwamba kwetu ni zaidi ya hapo. Mwaka jana lilitupa kipimo sahihi kuelekea EALA 2021, ambako tuliibuka washindi wa jumla katika michezo nane tuliyoshiriki. Tunatarajia kurejea mafanikio hayo mwaka huu kupitia bonanza hili," amesema.

Tarimba ambaye pia ni Mbunge wa Kinondoni, Dar es Salaam, alieleza kuwa wabunge, wafanyakazi NMB na waalikwa watakaohudhuria hafla ya usiku baada ya bonanza watapata fursa ya kuangalia kupitia televisheni kubwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC 2022/23), kati ya Yanga na Zalan FC ya Sudan Kusini.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, awali aliushukuru uongozi wa Bunge SC na manahodha wa timu za michezo yote, kwa kuipa nafasi NMB ya kuendelea na msimu wa pili wa bonanza hilo, ambalo hubeba fursa mbalimbali sio tu kwa Bunge, bali taasisi zingine za Serikali.

“Bonanza litaanza saa 12 asubuhi kwa matembezi yatakayoanzia Viwanja vya Bunge hadi Chinangali Park itakochezwa michezo mbalimbali, kuthibitisha faida za bonanza hili, tukifika pale tutakabidhi vifaa kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru, vyenye thamani ya shilingi milioni 50 na baada ya hapo, ndipo Kivumbi na Jasho kitakapoanza,” alieleza Mbunge huyo..

“Program hii ya Kivumbi na Jasho tuliianzisha mwaka jana, na tuwahakikishie wabunge kwamba bonanza hili litakuwa endelevu, na hii yote ni katika kuhakikisha kwamba tunaendeleza mashirikiano mazuri yaliyopo baina yetu na Wabunge, Ofisi ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Zaipuna alibainisha kwamba michezo ni afya, ni biashara, ni ajira. Lakini pia ni kazi na kwamba ushiriki wa wabunge - ambao ni wawakilishi wa wananchi, unatoa na kuakisi taswira ya umuhimu wa michezo kwa taifa na vijana kwa ujumla, huku akiwakaribisha wakazi wa Dodoma kuhudhuria bonanza hilo.

Vifaa vilivyokabidhiwa kwa timu za bunge ni pamoja na ‘track suit’ maalum na jezi za soka, netiboli, wavu, kikapu. Baadhi ya michezo itakayoshindaniwa, ni mpira wa miguu, mikono, kikapu, wavu, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mbio za magunia, mbio fupi na mingineyo, ambapo washindi watakabidhiwa vikombe na medali

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango