Shekimweri TAKUKURU aiipa njia kukabili rushwa

NA SAIDA ISSA,DODOMA

TAASISI ya Kuzuia na Kuapambana na rushwa Tanzania (TAKUKURU), imeshauriwa kuwajengea uelewa watumishi wa umma hasa katika maeneo ya manunuzi ili miradi inayofanyika iendane na thamani halisi ya fedha kudhibiti vitendo vya rushwa.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, alipotembelea maonesho ya ya maadhimisho ya Miaka 20 ya kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora yanayoendelea katika viwanja vya Jakaya Kikwete ambapo Taasisi mbalimbali za msaada wa sheria zinashiriki.

“Lazima tukiri kwamba kuna changamoto kwenye mapambano dhidi ya rushwa, kitu cha kwanza kumlea samaki akiwa mchanga kwani mnafanya kazi nzuri na kwenye wilaya tumeandaa  midahalo  kushindanisha shule kwenye kupinga masuala ya rushwa kwa njia ya mdahalo,” alieleza Shekimweri.

Alieleza kuwa hatua hiyo imelenga kujenga uelewa wa wanafunzi na kujenga tabia ya ya kuchukia vitendo vya rushwa wakiwa wadogo ili wawe raia wema siku za baadae.

Aidha Shekimweri aliwataka wananchi kujitokeza kupata elimu juu ya haki mbali mbali zinazowahusu inayotolewa na taasisi hizo pamoja na huduma zinazotolewa bila ya malipo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Bunadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji mstaafu Mathew Mwaimu, alisema kuwa tume wamekua wakipokea malalamiko toka kwa wananchi ikiwemo ya migogoro ya ardhi, rushwa, ubambikiwaji kesi na mateso kwa jeshi la polisi na taasisi nyengine za umma.

“Malalamiko yanayohusu migogoro ya ardhi yanayoletwa kwetu kwa sasa yamepungua lakini yale machache  yanayotufikia tunayashughulikia kwa kufanya uchunguzi na kutoa mapendekezo kwa taasisi husika na hatua zinachukuliwa hatua,” alieleza Jaji Mwaimu.

Kuhusu masuala ya unyanyasaji, Jaji Mwaimu alieleza kuwa yanapofikishwa tume na katika jeshi la polisi hufikishwa katika dawati la jinsia ambalo huanzisha mchakato wa upepelezi kabla ya kuyafikisha mahakamani.

Aidha jaji mwaimu aliwasihi watendaji wa taasisi za umma na binafsi na wananchi kwa ujumla kuzingatia na kuheshimu misingi ya haki za binadamu na utawala bora ili kwenda sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo ‘Miaka 20 ya kuhamasisha ulinzi wa hifadhi ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora’.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango