SMZ yaweka sawa taarifa kuhusu Mkurugenzi ZIPA

NA ABOUD MAHMOUD

SERIKALI imekanusha taarifa zilizozagaa mitandaoni zinazomuhusu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Shariff Ali Shariff, kuhusishwa na tuhuma za ujasusi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga,  katika Ofisi za Mamlaka hiyo, huko Maruhubi wilaya ya Mjini Unguja, alisema tuhuma hazina ukweli wowote na zimelenga kumchafulia jina mtendaji huyo  mzalendo kwa nchi yake.

Alieleza kwamba tuhuma zinazohusiana na mtendaji huyo kuwa na hati mbili za kusafiria zinaonekana kuwepo kwa watendaji wasio waaminifu wenye kuchezea mifumo ya nyaraka za Serikali.

"Kitendo kilichofanywa cha kumchafua mtendaji huyu sio kizuri kwani ni cha uongo hivyo hatutokua tayari kuona watendaji wanaharibiwa majina na naahidi uchunguzi kwa hatua zaidi,"alisema.

Aidha Soraga aliwaomba wandishi wa habari kuacha kuyatumia vibaya majukwaa yao na kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia miko na maadili.

Nae Shariff  aliitaka jamii pamoja na wana habari kufanya uchunguzi kabla ya kusambaza taarifa ili kujua ukweli na sio kutoa shutuma zisizokua na uhakika.

Alisema si vyema kukurupuka na kuanza kusambaza habari za kumchafulia mtu bila ya kuwa na uhakika.

Tuhuma zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zinamuhusisha Mkurugenzi huyo na mdogo wake ambae ni pacha anaeishi Jamuhuri ya watu wa Czech.

Ndugu yake huyo alikuja nchini na familia yake ambapo alipoondoka na kuonekana hati yake ya kusafiria ya nchi anayoishi zikasambazwa taarifa kuwa mtendaji huyo ana hati za uraia wa nchi mbili tofauti.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango