SMZ yajidhatiti kusimamia haki, ulinzi wa watoto
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema imejipanga kuimarisha ulinzi na kusimamia upatikanaji wa haki za watoto katika ngazi ya jamii.
WAZIRI wa Maendeleo, Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto, Riziki Pembe Juma (pichani), alieleza hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi wakati wa sherehe maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa (UN) yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Unguja.
Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda haki, fursa na kuimarisha ustawi na maendeleo hasa katika upatikanaji wa haki za watoto pamoja na kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
Amesema mikakati huo utakuwa pamoja na kuwajengea uwezo wa kisheria wanawake ili waweze kulinda na kusimamia haki na mambo mengine ya msingi ya nayo stahiki kupatiwa watoto.
Mbali na hilo amesema Wizara hiyo itafanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa kwa kuhimiza na kushajihisha wanawake kushiriki katika mchakato wa uchaguzi ili kushika nafasi ya uongozi katika siasa.
“Miongoni mwa mambo yatakayopewa kupaumbele ni pamoja na kuongeza nguvu katika kubadilisha mtazamo ya kijamii kisasa na kiuchumi kwa wanawake ili waweze kutumia fursa za maendeleo nchini,” amesema Waziri Pembe.
Katibu ya Jumuiya ya Kusimamia Haki na Malezi ya Watoto, Abdulkadir Nassor, amesema ulinzi wa watoto unahitaji nguvu za pamoja baina ya serikali na wananchi kwa jumla.
Amesema serikali imefanya juhudi za kuweka sheria na miongozo ya Kusimamia na kupatikana haki za watoto jambo muhimu ni mashirikiano na uwazi ndani ya jamii na watendaji.
Nae mkaazi wa Gongoni, Fatma Abeid, amesema moja ya changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa haki na ulinzi wa watoto ni ukiukwaji wa maadili na silka za Mzanzibari.
Comments
Post a Comment