Uzalishaji sukari kufikia tani 756,000 mwaka 2025

NA SAIDA ISSA, DODOMA

SERIKALI imesema imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa sukari   kutoka tani 380,000 inayozalishwa sasa nchini hadi tani 756,000 ifikapo mwaka 2025.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa  Bodi ya Sukari  Tanzania, Profesa Kenneth Bengesi (pichani) alipokuwa akielezea  muelekeo  wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo  kwa mwaka wa fedha  2022/ 2023.

Alieleza kuwa mpango wa serikali ni kuhakikisha kwamba mpaka ifikapo mwaka 2025/2026 nchi inakuwa na sukari ya kutosha pamoja na ongezeko  la viwanda vya  kuzalisha sukari.

Alisema miaka ya nyuma nchi ilikuwa inaagiza sukari hadi tani 183,000 lakini serikali imefanya juhudi zilizopunguza uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi kutoka tani 144,000 mwaka 2017 hadi tani 50,000 kufikia Juni, 2022.

“Tangu tupate uhuru, ndio tumepata wawekezaji katika upande wa sukari ikiwemo kiwanda cha sukari Bagamoyo na cha Mkulazi kinachotarajiwa kuanza mwaka 2023. Kuna upanuzi mkubwa wa kiwanda cha Kilombero utakaoongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 130,000 hadi kufikia tani 271,000," alisema.

Pia alisema uwekezaji wa kiwanda cha Sukari cha Kilombero umefikia zaidi ya shilingi bilioni 500 ambapo serikali ina asilimia 25 ya hisa katika umiliki wa kiwanda hicho.

Aliongeza kuwa kiwanda cha sukari cha Kagera kinaendelea na upanuzi ambapo kwa sasa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 140,000, ifikapo 2025/2026 kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 170,000.

“Kiwanda cha sukari Mtibwa nacho kinatarajia kuongeza uzalishaji kutoka tani 48,000 za sasa hadi tani 100,000 ifikapo mwaka 2025/2026,TPC kwa sasa inazalisha tani 100,008 na wana uwezo wa kufikia tani 120,000 na kiwanda cha Manyara kinazalisha tani 8,000 kwa sasa na kinatarajiwa kuzalisha tani 10,000 kwa mwaka 2025/2026,” alisema.

 Alifafanua kuwa kupitia viwanda hivyo  uwezo kutakua na uzalishaji wa tani 380,000 za  sukari kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo uzalishaji wa sukari kwa ajili ya matumizi ya viwandani haujaanza kufanyika na viwanda vya hapa nchini.

“Serikali ya awamu ya sita imeweka msukumo mkubwa na mazingira mazuri katika kuhakikisha tunaelekea kuzalisha sukari ya matumizi ya viwanda, tayari kuna wawekezaji wameshaanza kuonesha nia kwenye eneo hilo,” alisema Profesa Bengesi.

Wakati huo huo alisema kuwa takwimu zinazoishia Juni, 2022, mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida yaliyotumika kwa mwaka mzima ni tani 440,000 na sukari ya matumizi ya viwanda iliyoagizwa kutoka nje ni tani 205,000.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango